Michezo

Afya Bora Huimarisha Utendaji kazi – Waziri Jafo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo ameongoza zoezi la kufanya mazoezi kwa watumishi wa wizara hiyo na taasisi zake huku akitoa wito kwa watanzania kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi.

Mazoezi hayo yamelenga kujenga afya kwa Watanzania na kujiondoa katika hatari ya kukumbwa na magonjwa nyemelezi ambapo michezo ya Soka, Riadha, kutembea kwa kasi na Kuvuta kamba ilishirikishwa.

Akiwa ameambatana na Viongozi wengine waziri Jafo alikuwepo pia Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Joseph Kakunda, Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt.Zainab Chaula, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deogratius Ndejembi na baadhi ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Dodoma, pia baadhi yakazi wa Manispaa ya Dodoma.

Akizungumza wakati wa mazoezi hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma, alisema watanzania wanatakiwa kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuiweka miili yao vizuri, huku akitoa agizo kwa  ofisi yake kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi mara moja kwa mwezi ili kujenga afya zao pamoja na kufahamiana.

“Haya mazoezi tunamuunga mkono Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, katika juhudi zake za kufanya mazoezi, mazoezi ni muhimu kwa afya sasa kila mwezi tutakuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi  mara moja kwa mwezi ili kuongeza hamasa ya kufanya kazi,”alisema.

Naya Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kakunda alitoa dua maalum ya kuombea wote waliohudhuria, Mhe. Rais John Magufuli na kumshukuru Mhe. Jafo kwa kuandaa bonanza hilo ambalo lilileta hamasa, upendo na mshikamano wa watumishi Umma na watanzania.

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia Afya, Dk.Zainabu Chaula alimshukuru waziri kwakuwa mstari wa mbele katika kuonesha njia kwa watumishi suala linalo wajengea watumishi ujasiri na kuongezea ari ya utendaji kazi wao.

Akitoa salama za Mkoa,  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Mahenge alisema kutokana na Mkoa huo kuwa Makao Makuu ya Nchi ni lazima kuwe na viwanja bora vya Michezo.

“Mheshimiwa Rais ameanza ujenzi wa Uwanja wa michezo wa Kisasa katika eneo la Nzuguni  lazima tumuunge mkono kwani tunataka Mkoa wa Dodoma uwe wa kuvutia hivyo ni lazima kuwe na viwanja vingi vya michezo.

Taasisi zilizo shiriki ni Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI), Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Mfuko wa Pension wa LAPF, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa (LGLB), Wakala wa Barabara za Vijijini(TARURA) na Shirika la Elimu Kibaha (KEC), sambamba na wafanyakzi wa Mkoa na Halmashauri wa Dodoma na idara zingine za serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *