Habari za Wizara

Busega wapongeza ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya Nasa

 

Jengo la Upasuaji lilojengwa katika Kituo cha afya cha Nasa Kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.
 
Angela Msimbira OR-TAMISEMI Simiyu
 
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu wameishukuru Serikali kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ongezeko la watu Duniani UNFPA na KOIKA kwa kujenga jengo la Upasuaji, Wodi ya Wazazi, Nyumba ya Mtumishi na kisima kirefu cha maji katika Kituo cha Afya cha Nasa.
Pongezi hizo wamezitoa hivi karibuni wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa ujenzi wa majengo ya Wodi za Wazazi, Jengo la Upasuaji na nyumba ya mtumishi iliyojengwa katika Kituo cha Afya cha Nasa kilichopo katika Halmashauri ya Busenga Mkoani Simiyu chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ongezeko la Watu Duniani UNFPA na KOIKA.
Wananchi hao wamesema kuwa huduma hiyo itawasaidia akinamama wajawazito ambao walikuwa wakitembea umbali wa kilometa kilometa 40 kupata huduma za afya jambo ambalo lilikuwa likipelekea wengi kufariki kabla ya kupatiwaa huduma ya afya.
 
Wameipongeza Serikali kwa kusogeza huduma za Upasuaji kwenye maeneo ya karibu ambapo wakinamama wajawazito ambapo kwa sasa watakuwa wakitembea kwa umbali wa kilometa moja kupata huduma hizo za afya na kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
 
Akifafanua zaidi Bw. James Engalika amesema Serikali ya awamu ya Tano inajali wananchi kwa kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya nchini hasa kwa watu maskini ambao walikuwa wakikosa huduma za afya katika maeneo ya karibu lakini kwa sasa miundombinu ya afya imeweza kuboreshwa kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
 
Bw. Engalika ametoa wito kwa jamii hasa maeneo ambapo ujenzi wa vituo vya afya unaendelea kujengwa kusimamia na kujitoa katika kuchangia nguvukazi ili vituo hivyo viweze kukamilika kwa wakati na kuweza kutoa huduma za afya kwa jamii kwa kuwa maendeleo hayaletwi na Serikali pekee bali kunahitajika ushirikiano kutoka kwa wananchi.
 
“Ili kuleta maendeleo nchini, Wananchi wanatakiwa kufanya kazi kwa kujitolea kwa asilimia 90 lengo likiwa ni kupunguza changamoto za utoaji huduma za afya kuanzia ngazi za nchini hasa kwa wananchi maskini. “ Anasema Bw. Engalika
 
Amesema kuwa ushirikiano wa pamoja na mshikamano katika kujitolea huleta maendeleo kwa jamii na kuisaidia Serikali kutoa huduma bora za afya kwa jamii, hivyo kutokana na mshikamano uliokuwepo Kituo cha Afya cha Nasa kimeweza kukamilisha ujenzi wa jengo ya Upasuaji, Wodi ya Wazazi na nyumba ya Mtumishi kwawakati.
 
Naye Bi Eliza John mwananchi kutoka kijiji cha Nyanzima Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu anasema kuwa wakinamama wajawazito walikuwa wakiteseka sana wakati wa kujifunga kutokana na kutembea muda mrefu kufuata huduma za afya jambo ambalo lilipelekea kupata madhara makubwa wakati wa kujifungua akini kwa sasa wataweza kupata huduma bora karibu na maeneo yao.
 
Wakati huohuo Bw. Faraji Maiga Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Nasa amesema kuwa kituo hicho kilipokea fedha kutoka UNFPA shilingi Milioni 200 kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba ya Mtumishi, Wodi ya Wazazi na Chumba cha Upasuaji na serikali iliweza kutoa shilingi Milioni 250 kwa ajili ya Ujenzi wa Chumba cha kuifadhia maiti na maabara.
 
Amesema kabla ya ujenzi wananchi walikuwa wakipata shida ya matibabu lakini kwa sasa huduma za afya zitapatikana kwa kiwango kikubwa tofauti na kipindi cha nyuma ambapo wananchi walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma kwa kuwa hakukuwa na hospitali, hivyo wananchi wengi wanategemea huduma kutoka katika kituo cha afya cha Nasa.
 
Aidha amewashukuru wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Busega kwa moyo wakujitoa na kuweza kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya cha Nasa kwa wakati na aliwaasa wananchi wote ambao hawashiriki katika shughuli za maendeleo kushiriki kikamilifu kwa kuwa Serikali inatekeleza miradi kwa manufaa ya jamii.
 Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wakichangia nguvukazi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya cha Nasa kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.
Mratibu wa mradi wa RMNCAH- UNFPA Idara ya Afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Bi. Dinah Atinda akikagua jengo la nyumba ya Mtumishi katika Kituo cha afya cha Nasa Kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *