Habari za Wizara

Chaula ataka Mikoa Kuhuishwa na Mfumo Mpya wa MUKI

Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Dkt. Zainab Chaula akiongoza kikao kazi kuhusu Mfumo wa Ujifunzaji wa Kieletroniki (MUKI), baadhi ya wajumbe wake ni Menejimenti ya OR TAMISEMI, PS3,  Chuo Kikuu Huria cha TAnzania na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI) Jijini Dodoma leo

Na. Magdalena Dyauli na Fred kibano

Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Dkt. Zainab Chaula, ameshauri wawezeshaji wa Mfumo wa Ujifunzaji wa Kieletroniki (MUKI), kuusambaza mfumo huo katika mikoa yote bila kubagua ili kupata Viongozi bora kutoka mikoani.

Chaula ameyasema hayo leo wakati wa kikao kazi cha uwasililishaji wa matumizi ya Mfumo wa Ujifunzaji Kieletroniki (MUKI) Ofisini kwake Ofisi ya Rais TAMISEMI Jijini Dodoma.

“Mfumo wa Ujifunzaji wa Kieletroniki uende mbali Zaidi, viongozi wakuu wa Serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lazima waujue ili kuhakikisha mfumo unaimarika na kuleta tija”, alisema Dkt. Chaula.

Ameshauri mafunzo hayo yawe ya lazima kwa madiwani wote nchini mara baada ya kuchaguguliwa ili kuhakikisha uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano ya uongozi wao.

Naye Kiongozi wa timu ya Utawala Bora wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Dkt. Peter Kilema, ambao pia wamefadhili mradi huu, amesema mradi huo ambao ulibuniwa na Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Tanzania ili kuboresha mifumo ya sekta ya Umma nchini pamoja na Mfumo wa Ujifunzaji wa Kieletroniki (MUKI) ili kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Naye Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Dkt. Martin Madale alisema chuo hicho kimeshirikiana na Chuo kikuu Huria, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) kuwezesha Mfumo wa Ujifuzaji wa Kieletroniki kwa madiwani nchini.

“Awali mafunzo hayo yalikua ni ya ana kwa ana jambo ambalo lilileta changamoto ikiwemo gharama za kuwawezesha madiwani kushiriki mafunzo na uharibifu wa mazingira” alisema Dkt. Madale.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Chuo kikuu Huria Dkt. Edephonce Ngemera, alkiwasilisha mada ya mfumo huo, amesema mfumo huo utakuwa rahisi kutumia kwani umetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na pia halmashauri zitachaguliwa watu maalum wakiwemo maafisa TEHAMA ili kutoa mafunzo stahiki kwa madiwani watakaojifunza kupitia mfumo huo.

Akitoa mchango wake wakati wa kikao hicho Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Mhina alisema wanahakikisha mafunzo haya ya madiwani yawe endelevu katika halmashauri zote nchini na kwa halmashauri ambazo hazipo kwenye mradi wa PS3 ili kusukuma uwezo na utawala bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *