Habari za Wizara

Dkt. Chaula awapa somo wadau wa afua ya vipimo na tiba ya Malaria

Naibu Katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR –TAMISEMI), Dkt. Zainabu Chaula akizungumza katika Kikao cha Wadau wa Afua ya Vipimo na Tiba ya Malaria na Wataalamu wa Idaraya Afya OR-TAMISEMI leo Jijini Dodoma.

Na.Majid Abdulkarim

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Afya Dkt. Zainabu Chaula amewataka Wadau wa Afua ya Vipimo na Tiba ya Malaria na Wataalamu wa Idara ya Afya kuwekeza katika utekelezaji wa afua ya uangamizaji wa viluwiluwi wa mbu waenezao malaria “Larviciding”

Dk. Chaula amebainisha hayo leo jijini Dodoma katika kikao cha Wadau wa Afua ya Vipimo na Tiba ya Malaria na Wataalamu wa Idara ya Afya OR-TAMISEMI kilichofanyika katika ukumbi wa Refum, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Dkt. Chaula amesema kuwa ili kufikia lengo la kutokomeza Malaria lazima tutambue tumetoka wapi, tuko wapi na tunaenda wapi kwa kufanya tathmini kupitia takwimu zilizopo na kufanyia kazi baada ya kujua takwimu za sasa.

“Tumepewa dhamana na majukumu ya kuwatumikia watanzania hivyo ni wajibu wetu sote tulopewa majukumu kuhakikisha tunawatumikia watanzania kwa usawa ili kila moja aweze kufikia lengo kwani adhima yetu ni moja kama watanzania” Alisema Dk. Chaula.

Dkt. Zainabu Chaula amewataka wadau wote walioshiriki kikao hicho kuwekeza rasilimali fedha katika utekelezaji wa Afua ya Vipimo na Tiba ya Malaria ili kupunguza maambukizi ya Malaria nchini.

Dkt.Chaula amewataka kuwa wawazi, kuongeza ushirikiano na usawa baina ya Wadau, Waratibu wa Malaria Mikoani na Wilayani na Idara ya Afya OR-TAMISEMI ili kujua nini kina fanyika, wapi na wakati gani na nani anafanya nini kwa nafasi yake ili kuleta utendaji bora katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.

Naye a Kaimu Mkurugenzi Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR-TAMISEMI Jumanne Mwasamila amesema kuwa wamepokea maagizo na watayafanyia kazi  kwa lengo la kuhakikisha wanafikia malengo katika kutokomeza Malaria nchini.

Wakatihuohuo Mratibu wa Malaria na Uthibiti wa Mbu anayebeba vimelea vya Malaria “Vector Control” kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi. Stella Kajange amesema kuwa lengo la kikao hicho ni  kuwasilisha kazi wanazofanya katika utekelezaji wa Afua za matibabu na vipimo vya Malaria.

“Kupata tathimini ya matarajio yaliyofikiwa na ambayo hayajafikiwa kutafutiwa njia bora za utekelezaji ili yaweze kufikiwa na kuhakikisha tunatokomeza Malaria” Alisema Kajange.

Aidha kikao hicho kilihudhuriwa na Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe, National Malaria Control Program (MNCP), Wataalamu wa Idara ya Afya OR-TAMISEMI, Waratibu wa Malaria Wiliaya za Chamwini, Geita, Kibondo na Kasulu, Clinton Health Accesses Initiative, (CHAI), USAID Boresha Afya, SHOP PLUS na GHSC.

 

Baadhi ya Wadau wa Afua ya Vipimo na Tiba ya Malaria na Wataalamu wa Idaraya (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali (OR-TAMISEMI) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Afya) OR-TAMISEMI(hayupo pichani) leo jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *