Habari za Wizara

Dkt. Chaula : Kituo cha afya cha Nzera kimejengwa kwa viwango

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula akimsalimia mgonjwa anayepatiwa huduma ya matibabu katika Kituo cha afya cha Nzera kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita leo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ukarabati ba ujenzi wa vituo vya afya nchini.

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI GEITA

Naibu Katibu  Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula  ameipongeza Halmashauri  ya  Wilaya ya Geita  kwa kusimamia kwa weledi ujenzi wa kituo cha Afya Nzera kilichopo Mkoani Geita ambacho kwa sasa kinatoa huduma kwa jamii.

Akiwa kwenye ziara ya Kikazi Mkoani Geita Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa ameridhishwa na ukarabati pamoja na ujenzi wa kituo hicho kwa kujengwa kwa kuzingatia viwango vya hali ya juu  kwa gharama ya shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali.

“Nimeridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nzera ambapo mpaka sasa kimeweza kujenga majengo saba ya kutolea huduma ya afya ikiwemo duka la dawa, Chumba cha kuifadhia maiti, wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji, maabara na nyumba nne za watumishi” Anafafanua Dkt.Chaula

Dkt. Chaula amesema kuwa kufanya kazi kwa pamoja ndipo kulipofikisha hapo walipo na kuwezesha kituo hicho kukamilika kwa wakati na kuweza kuanza kutumia majengo hayo kwa ajili ya kutolea huduma za afya kwa jamii ya Halmashauri hiyo

Anaendelea kufafanua kuwa baada ya kufanya utafiti wa kina na  kugundua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina wakazi  7036 lakini katika wakazi hao  kulikuwa na vituo 5 vya afya  vilivyokuwa vikitoa huduma na vituo hivyo havikuwa vikitoa huduma stahiki za afya ndipo Serikali ilipoamua kuwekeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika kituo hicho.

Aidha amewapongeza wananchi kwa mchango mkubwa wa kuhakikisha kituo kinakamilika kwa wakati na kutumia nguvukazi katika ujenzi wa kituo hicho hivyo amewasisiriza kufanyakazi kwa umoja, mshikamano na  moyo wakujitolea ili kuunga mkono juhudi za  Serikali katika jitiada zake za kuleta maendeleo kwa jamii

Wakati huohuo mbunge wa Jimbo la Geita  Mhe.Joseph Kasheku Msukuma  ameipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha afya cha Nzera jambo ambalo limesaidia wananchi wa jimbo hilo kupata huduma za afya katika eneo la karibu wanapoishi tofauti na awali walikuwa  wanatembea muda mrefu kufuata huduma hiyo.

Amesema kuwa  kata zinazopata huduma za afya katika kituo hicho ni Kata ya Kubasa iliyoko umbali wa  kilometa 90  na Nkombe iliyoko  umbali wa kilometa 40, hivyo amemuomba Dkt. Zainabu Chaula kuongeza  vituo vya afya  katika maeneo hayo ili kuwapunguzia wananchi shida ya kutafuta huduma ya afya.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula akimsalimia mama aliyejifungua katika wodi mpya ya wazazi katika Kituo cha afya cha Nzera kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita leo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ukarabati ba ujenzi wa vituo vya afya nchini.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula akikagua jengo la duka la dawa katika Kituo cha afya cha Nzera kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita leo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ukarabati ba ujenzi wa vituo vya afya nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *