Habari za Wizara

Dkt.Chaula : Toeni elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Zainabu Chaula akikagua stoo ya dawa kituo cha afya cha Katoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoani Geita leo alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa vituo vya afya nchini.

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI  GEITA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Zainabu Chaula amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa bima ya afya nchini.

Dkt. Chaula ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ukarabati na ujenzi wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita.

Amesema kuwa Watanzania hawatafanikiwa kielimu na kiuchumi kama hawatakuwa na afya bora hivyo ni jukumu la viongozi wote nchini  kuhakikisha wanawahimiza wananchi kuwa na utaratibu wa kukata bima ya afya kwa ajili ya familia zao.

Amesema Bima ya afya inamsaidia mwananchi pale anapougua gafla na kukosa fedha za matibabu hivyo ni muhimu Wanganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa  kukata bima ya afya nchini.

“Inasikitisha kuona wananchi wengi hawajui umuhimu wa kukata bima ya Afya, nawaagiza Viongozi wote kutoa elimu ipasavyo kwa wananchi ili waelewe umuhimu wa kuwa na bima ya afya kwenye familia zao” Amefafanua Dkt. Chaula

Dkt. Chaula  amewaagiza viongozi hao kuwahimiza wananchi kukata bima ya afya kwa ajili ya kuimarisha afya zao  kwa sababu  ni muhimu na inasaidia familia  pindi zinazopata maradhi  na kuhitaji huduma za afya.

Kuhusu ukarabati na ujenzi wa vituo vya afya nchini Dkt. Zainabu Chaula amewapongeza wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa  kuchangia nguvu kazi  katika ujenzi wa vituo vya afya ili kuunga mkono juhudi za Serikali  na kusogeza  huduma za afya karibu na wananchi.

Dkt. Chaula amewahamasisha wananchi wa Kata ya Bwina, Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuchangia nguvukazi ili kuanza ujenzi wa Kituo cha afya cha eneo hilo ambacho kitaungwa Mkono na Serikali.

Amesema Serikali inajenga miundombinu ya afya kwa  kuchagua maeneo yaliyopo mbali na kuyajenga  kimakakati ili kuwapunguzia adha wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya  lengo likiwa ni  kuweza kutoa huduma  bora kwa jamii

Aidha Dkt. Chaula amekamilisha ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Geita ambapo ametembelea Vitio vya afya na Zahanati za Halmashauri ya Wialaya ya Geita na Chato Mkoani hapo.

Wodi ya wazazi iliyojengwa katika kituo cha afya cha Katoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoani Geita
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Zainabu Chaula akikagua eneo la kujenga kituo cha afya katika Zahanati ya Katete iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mkoani Geita leo alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa vituo vya afya nchini.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Zainabu Chaula akiongea na baadhi ya wagonjwa alipotembelea kituo cha afya cha Katoro kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mkoani Geita leo alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa vituo vya afya nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *