Habari za Wizara

Dkt. Gwajima Awaasa Watumishi Kuzingatia Sera ya Ugatuaji katika kazi zao

 

Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na watumishi wa kada ya afya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhusu utoaji wa hiuduma za afya kwa Watanzania kuanzia ngazi ya kijiji mpaka Taifa

   

KARIBU OR TAMISEMI – Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima alipowasili katika ofisi za wizara Jijini Dodoma leo

Na. Majid Abdulkarim na Fred  Kibano

Watumishi wametakiwa kuwa na uelewa wa kazi wanazofanya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa ili kuimarisha uratibu mzuri, uwazi, utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kufanya watanzania wajivunie uwepo wao katika nafasi hizo.

Hayo yamebainishwa leo na Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima wakati wa kikao chake cha kwanza baada ya mapokezi yaliyohudhuriwa na menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI jijini Dodoma leo.

 “Sisi watumishi ndio ramani ya watanzania kuweza kufikia chachu ya maendeleo ya nchii hii, hivyo tukiratibu na kutekeleza majukumu yetu kwa ufasaha ni haki yetu kupata matokeo chanya ya maendeleo ya nchi hii” Amesema Dkt.Gwajima.

Dkt.Gwajima amesema lazima serikali ijenge mfumo mzuri wa uratibu na utekelezaji wa majukumu yake kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa kwani ndio njia stahiki ya kuweza kupata Tanzania yenye maendeleo na kufanya watanzania kujifunia Utanzania wao.

Akiongea katika kikao cha menejimenti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI wakati wa kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu (Afya) Dorothy Gwajima, Kaimu Katibu Mkuu Tixson Nzunda Ofisi ya Rais – TAMISEMI), amesema ili mtumishi wa Umma aweze kutimiza majukumu yake ya kila siku ni lazima atambue kuwa yeye ni wakili wa anaowahudumia, mratibu wa matokeo chanya, awe mcheshi kwa jamii anayoihudumia na yeye ajihisi ni sehemu moja wapo ya jamii hiyo.

Katika hatua nyingine kwenye kikao maalum na watumishi wa Idara ya Afya, Dkt. Gwajima amewaasa watumishi wa Idara ya Afya Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuuvaa uhusika wa jamii wanayoitumikia katika kutekeleza majukumu yao ili kupata chachu ya kufanya kazi kwa ufanisi, juhudi na kutoa huduma bora kwa watanzania.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe amempongeza Dkt. Gwajima kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kwa niaba ya Idara yake ambapo ameahidi watampa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa na kwamba wapo tayari kupokea maelekezo yote ya Serikali.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Fedha katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa OR-TAMISEMI Miriam Mmbaga amesema kuwa ameguswa na mfumo aliokuja nao Dkt. Gwajima wa kutaka uratibu, uwazi, utekelezaji na ugatuzi wa madaraka kuanzia ngazi ya kijiji mpaka Taifa na kwamba utaleta chachu ya matokeo bora katika kutekeleza majukumu yao.

Dkt.Gwajima ameteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo jana kuwa Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *