Afya

Dkt. Gwajima Awakumbuka Yatima, Awapa mkono wa Eid

 

 

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (Afya), akiwa amembeba mtoto Queen Daudi Issa, wa kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya Matumaini cha mjini Dodoma, wakati Naibu Katibu Mkuu walipofika katika kituo hicho kwaajili yakutoa msaada kwa watoto hao kwaajili yakusherehekea Sikukuu ya EifFitr 2019(Picha na OR-TAMISEMI)

Na. Atley Kuni- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya (OR-TAMISEMI) Dkt. Doroth Gwajima akiwa ameambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Afya eneo la Ustawi wa Jamii Rasheed H. Maftah na wataalam wa Wizara hiyo wametekeleza utume huo kwa kutembelea kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya matumaini na kutoa misaada ya vitu mbali mbali wakati huu wa kuelekea sikukuu ya Eid Elfitr.


Akizungumza katika hafla yakukabidhi misaada hiyo, amekipongeza kituo hicho kwa jukumu kubwa walililo nalo lakuhakikisha watoto waliopo hapo wanapata malezi bora huku akiwaasa watoto kuzidisha upendo na mshikamano miongozi mwao.
“Tunatekeleza hili kwakuwa ni wajibu wetu kuwalea watoto kwani hata sisi leo tumekuwa watu wazima ni kwa sababu ya juhudi za wakubwa zetu, nanyi mtakuwa wakubwa kama sisi ili kesho na kesho kutwa mje kuwa viongozi wa taifa hili katika nyanja mbali mbali, hivyo kupendana na kuishi kwa amani ni suala muhimu sana” alisema Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya ustawi wa Jamii, OR-TAMISEMI, Rashhed H. Maftah, alisema zoezi hilo ni moja ya majukumu yao ya msingi na wajibu wao katika kuzihudumia Mamlaka zote 184 nchini katika kuhakikisha mtoto analindwa katika ngazi zote na kwamba hawatarajii kuona wala kusikia mtoto ananyanyasika kwa namna yeyote ile.
“Dini iliyosafi ni yenye kuwajali Yatima na wenye uhitaji kwa kuunganika na kushiriki nao katika mahitaji yao ya Msingi, aidha Sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kanuni ya 12 inahimiza suala la kulelea watoto” Alisema Maftah.
Akizungumza kwa niaba ya Walezi wa kituo hicho, mmoja ya walezi, Sister Urea, alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 63 na kimekuwa kikifanya kazi zake toka mwaka 1995 kwa kuhudumia watoto wanaopatikana katika mazingira magumu na ukatili wa kijinsia kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.
Akishukuru kwa niaba ya wenzake mtoto Mariah, alimshukuu Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake huku akiomba zoezi hili lisiwe la mwisho bali liwe endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika sana.
“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia misaada, lakini msiishie kuja kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na sisi, tunaomba Mungu awazidishie pale mlipotoa na siku nyingine tena mtukumbuke” alisema Mariah.
Kwa Mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii kutoka jijini Dodoma, kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Kata ya Mihuji ni moja kati ya vituo vinane vilivyopo ndani ya Halmashauri hiyo ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kulinda haki za watoto.

Vitu vilivyo kabidhiwa wakati wa hafla hiyo ni pamoja na Sabuni Kilogram 25, Mchele Kilogram 50, Mafuta Lt. 10 na Sukari Kilogramu 25. ambavyo vyote vitatumika kwaajili yakuwahudumia watoto hao.

Watoto wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini cha Mjini Dodoma, wakiimba Wimbo wa kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake kuwapa mkono wa Eid watoto wa kituo hicho
Picha ya Pamoja mara baada yakupokea misaada.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *