Habari za mikoani

Dkt. Tulia Kupamba Simiyu Festival 2018

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo kuhusu, Simiyu Jambo Festival inayotarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.  Dkt. Tulia Ackson anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio kubwa linalojulikana kwa jina la Simiyu Jambo Festival, ambalo linatarajiwa kufanyika Julai 8 mwaka huu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo kwa mwaka huu 2018 linafanyika kwa mara ya pili

Tukio  hilo ambalo litafanyika kwa mara ya pili, limebeba  vipengele vikuu vinne vya mashindano ambavyo ni mashindano ya  mbio za baiskeli, ngoma za asili (wagika na wagalu), mbio fupi kilomita 10 kwa wanaume na wnawake, mbio za uwanjani kwa watoto na uandishi wa insha yenye kauli mbiu yake ni Familia Yangu, Afya Yangu, Furaha Yangu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati ya uzinduzi wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka alisema tukio hilo, linalengo la kukuza vipaji kwa vijana wa Mkoa wa Simiyu na  kutangaza tamaduni za kabila la Kisukuma na kwamba litahusisha wananchi wote kutoka mikoa mbalimbali.

“Tutakuwa na mashindano ya mbio za baiskeli kilomita 150 wanaume, kilomita 100 wanawake, kilomita 11 watu wenye ulemavu,  mbio fupi za kilomita 10 wanaume na wanawake, mbio za watoto za uwanjani, uandishi wa insha kwa wanafunzi na  zaidi ya shilingi milioni 22 zitashindaniwa nitoe wito kwa Watanzania wote hususani vijana kuchangamkia fursa hii” alisema Mtaka na kuongeza

“Hii ni fursa pia kwa Wanasimiyu ambao ni wenyeji, sisi tunasema mbio za barabarani na uwanjani ni biashara , mashindano ya baiskeli ni biashara lakini kikubwa zaidi hili ni tukio ambalo litautangaza utamaduni wa Wasukuma wenye mvuto sana ambapo makundi mawili ya Wagika na Wagalu watacheza ngoma za asili na fisi na chatu, nitoe wito kwa watu wote kuja kuona haya.”

Mtaka alisema ushiriki katika mashindano ya mbio za baiskeli, ngoma za asili na uandishi wa insha ni bure isipokuwa mbio za kilomita 10 kwa wanawake na wanaume ambazo washiriki watatakiwa kulipa gharama ya shilingi 5,000/= kwa ajili ya usajili.

Naye Joseph Paulo Mwenyekiti chama cha Baskeli Mkoa wa Simiyu alisema kuwa uongozi mzima wa chama chao tayari wamejipanga ipasavyo kupokea na kusajili washiriki ambao watakuwa tayari kushiriki mashindano hayo ya Baiskeli kwa wanawake na wanaume.

Kwa upande wake Dkt. Amir Ibrahimu mwakilishi wa shirika la UNFPA, Mkoa wa Simiyu alisema shirika hilo limeamua kuwa ni moja ya wadhamini  wa Simiyu Jambo Festival waweze kufikisha elimu wananchi wa Simiyu na jamii yote  kwa ujumla itakayowasaidia kuona umuhimu wa uzazi wa mpango, kupinga mimba za utotoni na kuhamasisha kina mama wajawazito kujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua.

Aidha Akizungumzia zawadi kwa washindi watakao shiriki mashindano mbalimbali katika tukio hili la Simiyu Jambo Festival, Afisa Masoko wa Jambo Food Products Company ambao ndio wadhamini wakuu wa  mashindano hayo, Anthony Paul alisema kwa mwaka huu zawadi zimeongezeka hadi kufikia milioni 22.

Naye Mratibu wa mashindano hayo Zena Mchujuko alisema maandalizi yanaenda vizuri hivyo wananchi wote ndani ya Mkoa wa Simiyu na nje ya Mkoa wajitokeze kwa wingi kushiriki mashindano hayo.

Simiyu Jambo Festival mwaka  2018 inadhaminiwa na Jambo Food Products Company, UNFPA, Maswa Standard Chalks, Meatu Milk, NGS Petroleum Limited, Alliance Ginneries Ltd, NGM Gold Mine Limited, SIBUKA na Busega  Mazao Limited.

Mratibu wa Simiyu Jambo Festival, Bi. Zena Mchujuko akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya tukio hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Julai 08, 2018 mjini Bariadi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *