Habari za Wizara

Dodoma lazidi kuwa Jiji la Mfano

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mhe.Selemani Jafo(Mb) amesema Serikali itaendelea kutenga fedha na kuelekeza miradi ya Kimkakati katika Jiji la Dodoma ili Jiji hilo liweze kuwa bora kama yalivyo majiji mengine ya Kimataifa.
Waziri Jafo aliyasema hayo katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ushauri katika utafiti na usanifu wa mfumo wa utiririshaji wa maji ya mvua na maandalizi ya mpango wa uboreshaji wa mifumo ya mitaro ya maji ya mvua na maji taka katika jiji la Dodoma kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020 hadi 2040.
Jafo amesema kuwa Jiji la Dodoma linatakiwa kuendana na hadhi ya kamao makuu hivyo inahitaji fedha za kutosha za kuweza kuwekeza katika miundombinuyenye ubora itakayobadilisha sura ya Jiji.
“Hapa kunatakiwa kuwa na Maduka makubwa (Shoping Malls), Hoteli za hadhi ya nyota tano, majengo ya biashara, vivutio vya Utalii hata ikiwezakana patengenezwe bahari na fukwe za kupumzikia hii itafanya wananchi wa Jiji hili kupata huduma zote muhimu na kufurahia maisha wakati wote” Alisema Jafo.
Akizungumzia mkataba wa utafiti na usanifu amesema anachokitaka ni kuona mradi huu unajibu hoja za Wananchi wa Jiji hili kwa zaidi ya miaka ishirini ijayo kusiwe na changamoto katika eneo la maji taka na maji ya mvua.
Wakati huo huo, Waziri Jafo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi makini katika matumizi ya mapato hayo.
“Jiji la Dodoma ndiyo Jiji pekee linaloongoza kwa ukusanyaji wa pato ghafi kwa Halmashauri zote nchini lakini kukusanya ni jambo moja na kutumia ni jambo linguine nafurahia leo kuona mnasini mkataba miradi ya maji katika kata ya Hombolo hongereni sana kwa hilo.
Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amesema mradi huo utatoa suluhisho la kudumu katika kupambana na mafuriko ya mara kwa mara katika Jiji la Dodoma na utaweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa maji taka ili kuhakikisha mazingira ya jiji yanabaki kuwa nadhifu wakati wote.
Lengo la mradi huo ni kuandaa mpango jumuishi wa mifumo ya maji ya mvua na maji taka ambao utahusisha mifumo ya maji ya mvua, ukusanyaji wa maji taka kutoka kwenye ngazi ya kaya, usafirishaji salama kutoka kwenye makazi, uhifadhi pamoja na uchakataji kwa lengo la kubadili maji taka kuwa bidhaa nyingine kwa matumizi anuai yenye tija na salama kwa jamii
Mradi utatekelezwa na mshauri msanifu toka kampuni ya Cheil Engineering Co. Ltd kutoka Jamhuri ya Korea Kusini kwa kushirikiana na kampuni ya AJOMA Consult Ltd. ya Tanzania kwa mkataba wenye gharama ya Shilingi 1,575,573,813.10, ambao utatekelezwa kwa muda wa miezi 12 kuanzia tarehe Mei 6, 2019 mpaka Mei 5, 2020.
Aidha Mradi huu uko chini ya mradi mama wa Uendelezaji wa Miji Mkakati (TSCP) awamu ya pili unaosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *