Habari za Wizara

Elimu ya Msafa kuwajengea uwezo Madiwani

Dkt. Peter Kilima kutoka Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za umma PS3, akitoa maelezo kuhusu mafunzo ya Elimu kwa Masafa kwa Madiwani.

Na. Atley Kuni- OR TAMISEMI

Madiwani kote nchini wataanza kupata mafunzo ya uongozi kwa njia ya masafa kupitia mtandao wa kielektroniki, yaani kupitia mfumo wa intaneti, hali itakayowawezesha kujiimarisha katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwatumikia wananchi.

Akitoa mada katika mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini, Mhadhiri wa chuo Chuo Kikuu Huria, Dkt. Adephonce Fuka, alisema shabaha ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi katika maeneo yao.

Akizungumza wakati wa mawasilisho, Dkt. Fuka alisema nia kuu ni kuhakikisha Madiwani wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza mabaraza ya madiwani, na mafunzo hayo ni maboresho ya kitabu cha rejea ya Mh. Diwani kilichotumika kufundisha Madiwani kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa 93 hapo awali.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa kwa mtindo wa Elimu-Masafa ili kuwezesha kujifunza mahali popote, yataendeshwa na Chuo cha Serikali za Mitaa – Hombolo, na  ni marejeo ya mafunzo ya awali ambayo yalitolewa kwa viongozi hao kwa Halmasahuri 93 zilizopo chini ya mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kutolewa kwa wasilisho la elimu hiyo ya masafa kwa njia ya kieletroniki, mwakilishi kutoka PS3, Dkt. Peter Kilima, alisema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), unafanya kazi katika mikoa 13 na Halmashauri 93 na tayari umejipanga kutoa elimu kwa madiwani nchi nzima.

“Mradi huu ni wa miaka mitano, na moja ya maeneo tunayoimarisha ni mfumo ya Utawala Bora na Ushirikishwaji wa Raia.  Katika hili, Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo ndio wanaoongoza kipengele cha kutoa mafunzo kwa madiwani, kwa madiwani ndio wawakilishi wa wananchi walio ngazi ya chini kabisa,” alisema Dkt. Kilima.

Dkt. Kilima alisema kuanzishwa kwa utaratibu wa kufundisha kwa masafa (Mfumo wa Ujifunzaji Kielektroniki – MUKI) ni mafunzo yaweze kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi, gharama nafuu na kwa ufanisi zaidi, tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati wanaanza.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa madiwani yatajikita zaidi katika mada za historia na uhalali wa kisheria wa Serikali za Mitaa, sheria za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Muundo, Majukumu na Madaraka ya Serikali za Mitaa, sambamba na uendeshaji vikao vya kamati na mikutano ya Baraza.

Muongozo huo utakaokuwa unatoa elimu kwa masafa na kupatikana vilevile kupitia simu ya mkononi, utaangazia suala la utawala bora na ushirikishwaji wa wananchi, maadili ya madiwani, uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi shirikishi kwenye jamii, sambamba na usimamizi wa ardhi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Maeneo mengine ni, usimamizi wa raslimali watu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, usimamizi na udhibiti wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, wajibu, majukumu, haki na stahiki za Diwani, pamoja na masuala mtambuka katika jamii.

Hali ya Ulinzi na Usalama inapothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Gilles Muroto.

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa ALAT wa 34 unaoendelea mkoani Dodoma wakifatilia kwa makini mada zikitolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *