Mafunzo

FMO’s Wakumbushwa Utendaji wao

 

Dkt. Charles Mhina Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa wakati akifungua Semina ya Maafisa usimamizi wa fedha wa ngazi ya Mikoa (FMOs) katika Ukumbi wa OR TAMISEMI pembeni ni Mkurugenzi wa TEHAMA OR TAMISEMI Ndg. Erick Kitali.

Na Atley Kuni- TAMISEMI

Maafisa Usimamizi wa Fedha (Finance Management Officers – FMOs) kutoka Sekretarieti za Mikoa yote ya Tanzania Bara wamesisitizwa kuwa jicho la usimamizi wa fedha za Halmashauri na kutoa taarifa kwa Katibu Tawala (RAS) pamoja na ngazi ya Wizara ili kuwa na taarifa sahihi za kifedha kuanzia ngazi ya Halmashauri, Mkoa na Wizara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Charles E. Mhina wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Fedha zinazopelekwa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Fiscal Transfer Tracking Monitoring(FTTM) – Web Portal)  yanayowakutanisha FMOs kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia tarehe 27-28 Machi, 2018 kwenye ukumbi wa Maabara ya Kompyuta uliopo katika jengo la Sokoine OR TAMISEMI, mjini Dodoma.

Dkt. Mhina amewahimiza Wataalam hao kuwa eneo la utoaji wa taarifa ni muhimu sana ili kuwa na taarifa sahihi zitakazosaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.

“Tulichobaini kama Wizara kuna umuhimu wa kuimarisha daraja la mawasiliano kati ya FMOs na Halmashauri. FMOs mmekuwa mkitoa taarifa kwa RAS na Wizara, huku mkisahau kwamba nyinyi kama wataalam mnatakiwa kuzisimamia na kuzijengea uwezo Halmashauri pia.” amesema Dkt. Mhina na kuongeza kuwa changamoto zilizopo zianishwe na kutumika kama chachu yakuleta mabadiliko.

“Changamoto ya matumizi sahihi ya mfumo wa FTTM – Web Portal kutokana na ukosefu wa mafunzo imekuwepo toka 2015. Sasa tumieni fursa hii ya mafunzo mtakayoyapata kikamilifu ilimtakapo ondoka hapa mlete mabadiliko chanya katika usimamizi wa fedha. Wataalam wetu wa TEHAMA na FEDHA kutoka OR TAMISEMI wapo tayari na wamejipanga kuwaelekeza kikamilifu.” alisema Dkt. Mhina.

Pamoja Wataalam hao kusisitizwa juu ya mfumo wa FTTM-Web Portal, Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA OR TAMISEMI, Ndg. Erick Kitali  hakusita pia kuwakumbusha Wataalam hao kuwa ifikapo Julai Mosi, 2018 Mamlaka zote za Serikali za Mitaa zitumie  toleo jipya la 10 la Mfumo wa Malipo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa  (Epicor 10) ili kwenda sambamba na mahitaji ya sasa.

Ndg. Kitali amewaambia wataalam hao kuwa OR TAMISEMI katika utendaji wake wa kazi hutegemea sana ushauri wa Wataalam kutoka ngazi za msingi ambapo ndipo walipo wananchi. Hivyo, aliwataka Wataalam hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Erick Kitali Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA OR TAMISEMI, akisisitiza jambo kwa Maafisa usimamizi wa fedha wakati wa semina hiyo ya siku mbili mjini Dodoma.

 

Mmoja ya Maafisa wawezeshaji wa Semina hiyo kutoka OR TAMISEMI akitoa ufafanuzi wa awali kabla ya kuanza kwa semina hiyo ya siku mbili.

 

Shani Mangesho Afisa usimamizi wa fedha kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Tabora akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbali mbali kwenye mikoa wanayo yasimamia hususan ni masuala ya fedha.
Elisius Gujenji, Afisa fedha kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akieleza kwa kifupi majukumu yao kama wataalam wa fedha kwenye Mikoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *