Habari za Wizara

Halmashauri zaagizwa kutenga bajeti kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Waziri wa Nchi Ofisi YA Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. Selemani Jafo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watoto wenye matatizo ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

 

Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Mhe  Selemani Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini  kuhakikisha  katika mpango wa bajeti ya mwaka 2019/2020  kila Halmashauri kutenga shilingi milioni sita kwa ajili ya kuanza kushughulikia matatizo ya  watoto wenye kichwa kikubwa  na mgongo wazi nchini.

Ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi duniani iliyofanyika katika viwanja vya hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Jijini Dodoma leo.

Mhe Jafo amesema kuwa kila Halmashauri ikitenga fedha hiyo itasaidia kuhudumia watoto thelathini (30) jambo ambalo litakuwa linapunguza matatizo ya watoto hao nchini.

“Nahitaji  kuiona bajeti ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi  nchini  katika kila kitabu cha Halmashauri lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanapata tiba kwa wakati hapa nchini”anasisitiza Mhe. Jafo.

Akifafanua zaidi amesema Serikali imetenga fedha kupitia mapato yake ya ndani katika Hamashauri ambazo ni takribani bilioni 51 ambayo asilimia 2 ni kwa ajili ya vijana, asilimia 4 kwa  ajili ya kina mama na  asilimia 2 kwa ajili ya watu wenye ulemavu  lakini taarifa zinazotolewa na baadhi ya Halmashauri ni kuwa makundi ya walemavu ni machache.

“Nawaagiza Maafisa Usatwi wa Jamii kuhakikisha wanawatafuta watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kaya, kata, tarafa ili waweze kunufaika mna mikopo hiyo inayotolewa na Serikali, achene kukaa maofisini wahudumieni wananchi hasa watu wenye ulemavu” Anasema Mhe. Jafo

Amewaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kufanyakazi kwa uadilifu kwa kuwaibua watu wenye ulemavu waliofichwa majumbani ili waweze kupata haki zao za msingi zinazotolewa na Serikali.

Wakati huohuo amewataka Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha  wanawasilisha taarifa maalum kila mwezi  katika ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoelezea namna ilivyoweza kutatua matatizo ya watu wenye ulemavu katika Mikoa yao.

Amesema kuwa suala la watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi ni kubwa na linapaswa kusimamiwa hivyo watanzania waungane pamoja  ili kupunguza tatizo hilo na amewataka wazazi kuwa wajasiri katika kuwahudumia watoto  hao.

Amewataka Madaktari nchini kufanyakazi kwa weledi mkubwa kwa kujitoa katika kutoa huduma kwa jamii ili kuokoa maisha ya wananchi wanyonge na maskini.

Aidha amewataka Wakuu wa Mkoa wote nchini kusimamia kamati za watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha kwamba zinaundwa kwa ajili ya kuangalia kada zote za ulemavu.

Naye Mwenyekiti  wa chama cha ASBAHT Taifa  Bw. Abdulhakim Bayakub amesema changamoto kubwa ni uwepo wa vituo vichache vya kutolea huduma za watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, upungufu wa wataalam wa kutoa tiba hii pamoja na ukosefu wa vifaa tiba hasa mipira ya Shanti ambayo ndio mkombozi mkubwa wa watoto wenye vichwa vikubwa.

Aidha ameiomba Serikali na Hospitali zinazotoa huduma za watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kutoa mafunzo zaidi kwa madaktari katika Hospitali za Mikoani ili kufikisha huduma hii karibu na jamii na kupunguza msongamano katika hospitali zinazotoa huduma hiyo kwa sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. Selemani Jafo akimsikiliza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. James Kiologwe alipokuwa akielezea jinsi watoto wenye matatizo ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wanavyopatiwa matibabu kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na ngongo wazi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya watoto wenye vichwa vikubwa na ngongo wazi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa Mhe. Selemani Jafo akiangalia matibabu mtoto mwenye matatizo ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wanavyopatiwa matibabu kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *