Habari za Wizara

JAFO ahimiza uwajibikaji kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya

 

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akisistiza Jambo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika leo katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma.

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya  kusimamia ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea kote nchini pamoja na kuweka udhibiti imara wa upotevu wa fedha ili kusiwe na upungufu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma nchini.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na wa Halmashauri zote nchini uliofanyika katika ukumbi wa LAPF leo Jijini Dodoma.

“Fanyeni kazi kwa weledi kwani msipotimiza wajibu wenu ipasavyo tudumaza afya za wananchi, natamani itakapofika mwaka 2020 kila mwananchi azungumze faraja kwenye sekta ya afya”, alisema Waziri Jafo.

Aidha,Waziri huyo alisema katika ukusanyaji wa mapato hauridhishi,  hivyo kufanya vituo vingi kuwa na makusanyo madogo ya mapato ya kila siku licha ya kuwahudumia wananchi wengi.

Kwa upande wa kuboresha huduma za afya nchini, Waziri Jafo alisema wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kulikuwa na vituo vya afya 115 vilivyokuwa  na uwezo wa kufanya upasuaji wa dharura. Kwa sasa vipo vituo 210 ambavyo vinatoa huduma hiyo , sawa na asilimia 95

Aliendelea kufafanua kuwa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2018/2019 Serikali imetenga takribani bilioni 105 ambapo ajenda kubwa ni ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 hivyo kufanya vituo 307 vitakavyokuwa vinafanya upasuaji wa dharuara.

Waziri Jafo alisema kuwa uwepo wa vituo hivyo kutapunguza vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua na kupunguza changamoto za utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Aliwapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya kwa kuisaidia Serikali  kuokoa fedha katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya kwa kutumia taaluma zao ambazo zimesaidia kujenga vituo bora kulingana na mahitaji.

Amewaagiza washiriki hao kuhakikisha wanaongeza kasi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato katika Hospitali za Mikoa na Wilaya kwa kuhakikisha wanafunga mifumo ya kielektoroniki ya ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya), Mhe. Zainabu Chaula alisema ili kupunguza changamoto za afya nchini inabidi kufanyakazi kwa weledi, ushirikiano katika ngazi zote za uongozi, pamoja na wadau wa sekta ya afya nchini.

Amesema kuwa uwajibikaji wa pamoja na utumishi wenye weledi katika utoaji wa huduma za afya ndio msingi wa uboreshaji wa mazingira ya kutolea huduma za afya kuelekea Tanzania ya Viwanda na uchumi wa kati

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi. Mussa Iyombe amewaagiza watumishi wa Sekta ya afya  kutoka OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia  , Wazee na watoto kufanya kazi kwa weledi ili kuweza kutatua changamoto za afya kwa wananchi maskini wanaohitaji huduma katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya alihimiza umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi katika upangaji wa bajeti na mipango mingine ya sekta ya afya hususani kwenye vifo vitokanavyo na akina mama wajawazito na watoto wachanga kwani hivi sasa kila mwaka akina mama wajawazito wapatao elfu kumi na moja hufariki.

 Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Drk. Zainabu Chaula akitoa mada katika Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika leo katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akihimiza umuhimu wa matumizi ya takwimu afya kwenye Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika leo katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Musa Iyombe akisistiza uwajibikaji na ushirikiano kwa watumishi wa afya kwenye Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri uliofanyika leo katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *