Elimu

Jafo akemea vitendo vya Unyanyasaji na upendeleo wa walimu na wanafunzi

Na Mathew Kwembe, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewaagiza maafisa wa elimu wa mikoa na wilaya kuzingatia maadili kwa kuepuka vitendo vya upendeleo na unyanyasa wa walimu na wanafunzi.

Pia amewataka kujuepusha na suala la uvujishaji mitihani, rushwa na utovu wa maadili.

 

Katika hotuba yake ilisomwa na Naibu Waziri, Joseph Kakunda wakati wa kufungua kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha maafisa elimu wa mikoa na halmashauri kilichofanyika jijini Dodoma, Mhe.Jafo alihimiza umuhimu wa kuzingatia maadili na kusisitiza kuwa siku za hivi karibuni, sekta hiyo imejijengea picha mbaya kwa mambo kadhaa.

 “Tunatakiwa kuepuka vitendo vya upendeleo na unyanyasaji wa aina yoyote wa walimu na wanafunzi, uvujaji wa mitihani, rushwa na utovu wa maadili kwasababu ninyi ni kioo cha jamii,” alisema.

Jafo alionya kuwa vitendo vya utovu wa maadili kamwe havitavumiliwa na serikali na yeyote anayeendekeza vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali.

“ Nitumie fursa hii kulaani vitendo vya unyanyasaji na kiukatili vilivyofanywa na baadhi walimu katika shule ya msingi Kibeta iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.”

Aidha, Jafo aliwaasa viongozi hao kusimamia Sheria, kanuni na taratibu katika utoaji wa adhabu kwa wanafunzi kote nchini.

Jafo alitumia nafasi ya kutoa msisitizo kwa  viongozi hao kuwajibika katika kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuwajibika kwa umma, watumishi, wadau na marafiki wa elimu ili kuendeleza imani mliyoijenga kwa umma.

Aidha, Jafo alionesha imani kuwa mkutano huo ambao umewakutanisha watendaji wa elimu katika ngazi ya taifa, mikoa na halmashauri kwa lengo la kukumbushana majukumu, kujipima na kujitafakari utendaj , kupeana uzoefu, kujenga uwezo na kujadiliana juu ya minu na mikakati  itakayotumika kusaidia kuboresha utoaji wa elimu iliyo bora.

“Baada ya kikoa hiki hatutakuwa tayari kusikiliza watendaji mliopo hapa wala wasaidizi wenu mkitoa utetezi wa aina yeyote utakaosababishwa na uzembe katika utendaji ,” alisema.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *