Habari za Wizara

Jafo apiga marufuku Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwaswekwa ndani Madaktari

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akifunga mkutano wa hamsini wa taaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania uliofanyika leo katika ukumbi wa St. Gasper, Jijini Dodoma

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuacha tabia ya kuwasweka ndani madaktari bila ya kufanya tathmini ya makosa waliyoyafanya.

Akifunga Mkutano wa hamsini wa taaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania leo jijini Dodoma Mhe. Jafo amesema kuwa kitendo hicho kinadhalilisha taaluma ya udaktari na kuwavunja moyo watumishi hao katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Alisema kuwa kama daktari ana tuhuma yoyote inayomkabili iundwe tume ya kuchunguza makosa hayo kabla ya kumsweka ndani.

Waziri Jafo alifafanua kuwa baadhi ya vifo vinavyotokea hospitalini husababishwa na jamii kwa kuwachelewesha wagonjwa hospitalini lakini pindi kifo kikitokea tuhuma hizo hupelekewa daktari aliyemhudumia.

“Inasikitisha kuona baadhi ya wana familia wanamchelewesha mama mjamzito au mama mjamzito mwenyewe hajahudhuria kiliniki hata mara moja lakini kifo kikitokea daktari anawekwa ndani, hii si sahihi kabisa,” alisema.

Hivyo Waziri Jafo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuacha mara moja tabia hiyo ya kuwadhalilisha madaktari kwa makosa ambayo pengine siyo ya kwao.

Hata hivyo Mhe.jafo aliwataka madaktari hao  kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi katika kutoa huduma kwa jamii ili  kuacha alama katika maeneo yao wanayofanyia kazi.

Alisema kuwa taaluma ya udaktari ni muhimu katika jamii kwani husaidia kuokoa maisha ya watu hasa masikini hivyo ni vyema watendaji hao wakatumia taaluma yao vizuri ili waweze kukumbukwa na jamii kutokana na kazi nzuri walizozifanya.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt Obadiah Nyongole alisema kuwa mkutano huo unalenga kuwaleta pamoja wana taaluma ya udaktari ili waweze kujadiliana miiko na maadili ya taaluma ya udaktari na changamoto zake.

Aliongeza kuwa katika mkutano huo, madaktari walijadiliana namna bora ya kuwafikia wanyonge kwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha huduma tembezi za afya hasa maeneo ya vijijini.

Naye Mkurugenzi wa huduma za afya, Ustawi wa jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt Ntuli Kapologwe alisema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa taaluma hiyo imejenga nyumba 310 za kuishi za Madaktari katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Alisema kuwa japokuwa nyumba hizo hazitoshi kulingana na mahitaji lakini serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa inaboresha maslahi ya madaktari ili waweze kufanya kazi zao vizuri za kuwahudumia wananchi.

Baadhi ya Madaktari wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Hayupo pichani) wakati akifunga mkutano wa hamsini wa taaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania uliofanyika leo katika ukumbi wa St. Gasper, Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Afya Kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Zainabu Chaula akimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati akifunga mkutano wa hamsini wa taaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania uliofanyika leo katika ukumbi wa St. Gasper, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Madaktari wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Hayupo pichani) wakati akifunga mkutano wa hamsini wa taaluma wa Chama cha Madaktari Tanzania uliofanyika leo katika ukumbi wa St. Gasper, Jijini Dodoma.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *