Habari za Wizara

JAFO: Nitawatetea madaktari wanaotimiza wajibu wao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akiongea na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Concention Centre, Jijini Dodoma.

Na.Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo amesema kuwa atawatetea madaktari ambao watatimiza majukumu yao lakini hatasita kuwachukulia hatua wale ambao wataenda kinyumbe na taratibu.

Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya leo kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.

Mhe. Jafo amesema kuwa madaktari wamekuwa wakijitoa kwa weledi mkubwa katika kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa jamii na kuleta mabadiliko katika sekta ya afya  nchini.

“kuna watu wanafanyakazi usiku na mchana  tusipowalinda watu wanaofanyakazi  tutawaumiza,  siamini kama kweli mtumishi mmoja pekee anaweza kula fedha bila kuwa na ushirikiano na watu wengine, si kweli hata  kidogo, tutende haki kwa watumishi wanaotoa huduma za afya nchini” Amesisitiza Mhe. Jafo

Amesema Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaofanya vibaya wanapaswa kuadhibiwa lakini lazima haki itendeke katika kuwachukulia hatua ili kuleta usawa na kupunguza malalamiko kwa wataalam wa afya nchini.

Amewaagiza viongozi wa Halmashauri kutenda haki wakati wa kuwachukulia hatua watumishi kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina wa tuhuma zilizotolewa dhidi yao ili kujiridhisha ndipo watoe maamuzi  yaliyosahihi.

Mhe. Jafo anafafanua kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi kuwashusha madaraka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya  bila kufuata sharia na taratibu za kiutumishi kwa kusikiliza majungu na uongo usiofanyiwa kazi jambo hili si haki, hivyo serikali itaendelea kuwatetea na kuhakikisha wanarudishwa kwenye nafasi zao.

Naye,  Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu ya  huduma za afya ambapo  mpaka sasa vituo 470  vimekarabatiwa na kujengwa nchini  kwa gharama ya shilingi  bilioni 321.

Mhandisi Nyamhanga amewaagiza Wanganga Wakuu wa Mikoa na Wiilaya kuhakikisha wanasimamia utoaji wa huduma bora za afya kwa watumishi ili waweze kufanyakazi kwa bidi na kuhakikisha huduma za afya zinaboreka nchini.

Wakati huohuo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo na Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndungulile amewataka Wanganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha watumishi walio chini yao wanatoa huduma bora kwa jamii ili kuwavutia kupata huduma  hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya vilivyojengwa nchini.

Aidha Katibu Mkuu wa Afya, Maendeleo na Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainabu Chaula amewataka  Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya  nchini kuhakikisha wanafanyakazi kama timu kwa kudumisha umoja na ushirikiano ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa jamii zinakuwa bora nchini.

 Baadhi ya Waganga Wakuu wa Mkoa na Wilaya wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Concention Centre, Jijini Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi. Joseph Nyamhangaakiongea na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Concention Centre, Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akikagua mabanda ya maonesho ya wadau mbalimbali kwenye kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Concention Centre, Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *