Habari za Wizara

Kaaya awahimiza wananchi kutumia siku tatu kikamilifu kujiandikisha

Katibu Mkuu Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Bw. Elirehema Kaaya akijiandikisha kwenye Orodha ya Daftari la Wapiga Kura katika Mtaa wake wa Mlimwa Area D, Jijini Dodoma.

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Watanzania wametakiwa kutumia muda uliobaki wa  siku tatu kwa ajili ya  kujiandikisha katika orodha ya daftari la  wapiga kura ili kuweza kupata haki yao ya msingi ya kikatiba ya kugombea na kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 24 Novemba ,2019.

Hayo yamebainishwa leo na Katibu  Mkuu  Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Bw. Elirehema Kaaya  Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye  Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa mara baada ya  kajiaandikisha katika Mtaa wake wa Mlimwa Area D Dodoma.

Bw. Kaaya amesema kila Mtanzania anatakiwa kujiandikisha ili kupata haki yake ya kikatiba katika kugombea na kupiga kura kwa kuwa hakuna atakaye gombea au kupiga kura kama hajajiandikisha katika Daftari ya  Orodha ya wapiga kura katika eneo analoishi.

Amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka ambayo inasisitiza  Serikali  kupeleka madaraka ya kisiasa kwa wananchi ili waweze kuchagua viongozi watakaowasilisha  katika shughuli za kujiletea maendeleleo, hivyo ni haki yao ya msingi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kipindi hiki cha kujiandikisha ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kumchagua kiongozi ambaye atawaletea maendeleo kwenye mitaa, Vijiji na Kitongoji.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu  kwa vile unalenga kuwapata viongozi katika ngazi za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambao wataweza  kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Serikali Kuu, hivyo ni wajibu wetu sote kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha, kuchukua fomu na kupiga kura kwa kuwa ni haki kuchagua na kuchaguliwa”Amesisitiza Bw. Kaaya.

Wakati huohuo, Bw. Kaaya ametoa rai kwa watanzania wote nchini kutojihusisha na vitendo vya rushwa,ubaguzi wa kijinsia ,rangi na unyanyasaji wa aina yoyote  katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 24 Novemba, Mwaka huu ili kulinda amani na umoja wa wananchi katika kufikia malengo ya kuleta maendeleo ya taifa.

Aidha amesisitiza kuwa kila mtanzania anatakiwa kutambua kuwa kitambulisho cha mpiga kura hakitumiki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bali wajiandikishe katika Daftari la Orodha ya Wapiga kura kutokufanya hivyo kutakuondolea sifa ya kugombea na kupiga kura

Naye Mtendaji wa Mtaa wa Mliwa Bi. Getrude Festo, amesema zoezi  la kujiandikisha katika daftari la Orodha ya wapiga kura linaendelea  vizuri lakini changamoto kubwa ni kuwa  watu wengi kwa siku za kazi wanakuawa makazini, lakini kwa siku tatu zilizobaki wanaimani watajiandikisha ili wapate  fursa ya kupiga kura siku ya 24 Novemba,2019.

 

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mlimwa Area D Jijini Dodoma wakiendelea kujiandikisha katika Orodha ya Daftari la Wapiga ili kuweza kuwa na vigezo vya Kugombea na kupiga kura siku ya Tarehe 24, Novemba, 2019.
Katibu Mkuu Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Bw. Elirehema Kaaya akipokelewa na Mtendaji wa Mtaa wa Mlimwa Area D Bi. Getrude Festo leo Jijini Dodoma alipoenda kujiandikisha kwenye Daftari la Orodha la Wapiga Kura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *