Elimu

Kakunda ahimiza halmashauri ziwekeze kwenye michezo

Na Mathew Kwembe, Mwanza

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Mhe. Joseph Kakunda amesema wakati umefika sasa kwa Halmashauri kupitia mabaraza yao ya madiwani kutenga fedha kwenye bajeti zao kuwekeza kwenye sekta ya michezo.

Mhe.Kakunda ameyasema hayo hivi karibuni jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA ambapo alieleza kuwa halmashauri kupitia mabaraza ya madiwani zina fursa ya kuwekeza kwenye michezo kwani ni njia mojawapo ya kuinua uchumi wa halmashauri zao na taifa.

Alisema kupitia mabaraza hayo, halmashauri zinaweza kuwekeza kwenye michezo kwa kutenga bajeti ya kutosha ili kuendeleza uwekezaji huo.

Aliongeza kuwa mbali ya sekta ya michezo kuleta burudani katika taifa lakini imekuwa ni sekta muhimu kiuchumi huku akitolea mfano wa nchi ya Brazil ambayo kupitia sekta hiyo imeweza kuinua uchumi wake.

Pia mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yameliletea heshima kubwa taifa kwa kuibua vipaji vya wanamichezo mahiri.

“Matokeo ya mashindano haya yamedhihirika kwa kuwatoa wanamichezo mahiri mbalimbali kutokana na vipaji vyao walivyovionesha,” alisema.

Aidha, Mhe.Kakunda aliongeza kuwa wanataaluma na wanamichezo walioibuliwa kupitia mashindano hayo wamekuwa ni kioo cha taifa katika mashindano ya ndani na nje ya nchi na taifa kwa ujumla limepata heshima kubwa kupitia kwao.

Aliwataja baadhi ya wanamichezo hao ambao chimbuko lake lilianzia katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na Mbwana Samata, Edibily Lunyamila, Leodger Tenga na wengineo wengi ambao walionyesha umahiri mkubwa kwenye medani za kimataifa kwa kuliwakilisha vyema taifa katika mchezo wa mpira wa miguu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *