Mafunzo

Kakunda Awataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya Wapya kuacha Mivutano

Na. Magdalena Dyauli na Fred Kibano

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) anayeshughulikia ELIMU Joseph Kakunda amefungua rasmi mafunzo kwa Wakurugenzi wapya wa Halmashauri na Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni Jijini Dodoma leo.

Kakunda amewataka Viongozi hao kutambua kuwa wao ni tegemeo kubwa katika utekelezaji wa Sera za Serikali hivyo ni muhimu kujua wajibu wao, hasa kwa kuhimiza ushirikiano kwenye utekelezaji wa shughuli zinazolenga kuhudumua wananchi hapa nchini.

Aidha amewaagiza Viongozi hao kusimamia vyema suala la mimba za utotoni kwa kuwashughulikia wale wote wanaowaozesha na kuwapa mimba wanafunzi pamoja na kudhibiti utoro mashuleni.

Kakunda amewakumbusha pia kutumia busara katika kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo yao kwa kutumia nidhamu na haki lakini pia kusimamia mapato na kudhibiti fedha za Umma, kusimamia vyema amani na utulivu pamoja na kufanya kazi bila mivutano katika maeneo yao ya kazi.

Katika hatua nyingine ameipongeza Taasisi ya Uongozi ambayo dhima yake ni kuimarisha viongozi wa afrika ili matokeo ya uongozi wao yawapatie majibu endelevu dhidi ya changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania.

 “tangu ianzishwe taasisi hii ya uongozi imetoa mchango mkubwa kwa serikali kwa kutoa mafunzo  kwa viongozi wa ngazi mbalimbali” alisema Kakunda.

 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Zainab Chaula amewataka Viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) anayeshughulikia ELIMU Joseph Kakunda akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni Jijini Dodoma leo
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) anayeshughulikia ELIMU Joseph Kakunda akakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wapya wa Wilaya baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Dodoma leo

“naamini kila mtu alikabidhiwa ilani, yale ni mafunzo toshakama kila mmoja atayasoma na kuyazingatia”alisema Dkt Chaula.

Naye Kaimu Mkurugrenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi Kadeli Singo amesema tathmini iliyofanyika mwezi juni mwaka 2018 imeonyesha mafunzo hayo yamekua na manufaa makubwa kwa Viongozi waliohudhuria na kuleta tija katika kazi zao.

Mafunzo ya Uongozi kwa Awamu ya Tano yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi ni mwendelezo wa mafunzo kwa Viongozi wapya ambao huteuliwa na Mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *