Habari Kitaifa

 Katibu Mkuu Iyombe atoa neno zito Mkutano Mkuu ALAT

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe akisisitiza jambo kwenye Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) nchini ulioanza leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma uliowashirikisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini

Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Katibu Makuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe ameziagiza Halmashauri zote nchini  kuhakikisha wanajitathmini  katika utendaji  kazi wao hususani katika kuihudumia jamii.

Mhandisi Iyombe ameyasema hayo wakati akitoa mada kwenye Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) nchini ulioanza leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma uliowashirikisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini.

Mhandisi. Iyombe amewaagiza viongozi hao  kuhakikisha wanajibu hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali pamoja na maelekezo ya Kamati za Bunge kwa wakati ili kila Halmashauri iweze kupata hati safi.

“Serikali imekuwa ikitoa maagizo kuhusu kuhakikisha kila Halmashauri nchini inajibu hoja za Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali  lakini bado kuna Halmashauri nyingi hazijafanya hivyo, naagiza tena kuwa kila Halmashauri kuacha kulimbikiza hoja za wakaguzi na zihakikishe zinajibiwa kwa wakati” Amesisitiza Mhandisi Iyombe.

Wakati huohuo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanafanyakazi  kwa ushirikiano na kuacha tabia ya kuwagawa watumishi kwa maslahi binafsi badala ya kuangalia maslahi ya jami jambo linalo kwamisha shughuli za jamii

“Ushirikiano mdogo kati ya Wakuu wa Wilaya,Mameya/Wenyeviti wa Halmshauri na Wakurugenzi unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha  nyuma maendeleo katika Halmashauri nyingi nchini hivyo ni vyema wakafuata sheria na taratibu katika kufanya maamuzi katika utendaji kazi wao.

Ameendelea kufafanua kuwa kuna baadhi ya Halmashauri wanawagawa watumishi na kuleta majungu katika utendaji kazi wao jambo ambalo linasababisha kurudisha nyuma maendeleo katika Halmashauri na kushindwa kutoa huduma bora kwa jamii.

“Inasikitisha kukuta kuna watumishi wanaomsikiliza Meya/ Mwenyekiti na wengine kumsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri jambo hili si sahihi kwa kuwa huwezi kuongoza Halmashauri kama hakutakuwa na ushirikiano katika utendaji kazi’ Anasisitiza Iyombe

Hata hivyo amesisitiza kufuata sheria na taratibu katika kumuazimia mtumishi  kwa kuwa upo utaratibu wa kufuata  kama Mkurugenzi hatoshi kwenye nafasi yake kupunguza migogoro ya kiutumishi

Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia Mapato na matumizi  ya Halmashauri na kutoa nafasi kwa watumishi  kwa kuwasikiliza  kero zao lengo likiwa ni kujenga mahusiano mazuri katika utendaji kazi wao

“ Tengeni muda wa kuwasikiliza kero za watumishi na wananchi inasikitisha mtumishi anakuja mpaka Wizarani kufuatilia kero ambayo ingeweza kutatuliwa katika ngazi ya Halmashauri naagiza kero zote zitatuliwe katika ngazi ya Halmashauri.“Anasema Iyombe,

 Aidha amewaonya Wakurugenzi kutokusita kuwachukulia hatua maafisa Mipango wote  nchini  wanaoshindwa kuandika maandiko ya miradi  ya maendeleo ya kuzisaidia Halmashauri  zao   kwa ajili ya kuongeza  vyanzo vya mapato.

 

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mussa Iyombe leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma uliowashirikisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mussa Iyombe leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma uliowashirikisha Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini.

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *