Habari za mikoani

Kongole Ukusanyaji wa Mapato Kondoa Mji

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Mhe. Hamza Mafita akielezea jambo wakati wa kikao cha baraza

Na: Sekela Mwasubila A. Hbr Kondoa Mji

Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepongezwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2018/19 na kufikia asilimia 67 ya lengo la mwaka na kuwa halmashauri ya 3 kwa halmashauri za miji nchini.

Pongezi hizo zilitolewa na Bwana Peter Gujenji kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao cha baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Kondoa Irangi hivi karibuni.

Alisema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inatambua na inathamini juhudi zinazofanywa katika ukusanyaji wa mapato na inawapongeza sana kwa juhudi hizo na inandaa barua ya pongezi kulithibitisha hilo.

“Mwaka jana hadi robo ya pili inaisha halmashauri ya Mji ilikusanya milioni 200 sawa na asilimia 23 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2017/18 lakini kwa  kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 hadi robo ya pili inaisha halmashauri imekusanya zaidi ya shilingi 500 sawa na asilimia 67 kwa kweli mnastahili pongezi.” Alisisitiza Bwana Peter.

Aliongeza kwa kuwasihi viongozi wa halmashauri kuendelea kubuni mbinu zaidi za ukusanyaji wa mapato na kuongeza uwajibikaji na upendo ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mhe. Hamza Mafita alisema kuwa mapato yameongezeka baada ya kupata Mkurugenzi mpya kwakushirikiana kwa karibu na watendaji ambaye amewezesha kufikia hapo na hiyo imetokana na kufanya kazi kwa ushirikiano kati ya madiwani na menejimenti.

“Tumeongeza mashine za kukusanyia mapato hadi kufikia mashine 25 ambazo zimegawanywa katika kata mbalimbali kwa ajili ya kukusanya mapato na tuna mpango wa kufikisha mashine 50 ili kuhakikisha maeneo yote yenye mapato yanakusanywa.”Alisema Mhe. Hamza

Akielezea siri ya ukusanyaji wa mapato Mkurugenzi wa Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya watendaji na mikakati iliyowekwa katika ukusanyaji wa mapato.

“Tumeunda timu mbalimbali za ukusanyaji wa mapato kwa kuweka mameneja ambapo kuna meneja wa POS, masoko na mageti ya mazao pamoja na hizo timu pia tumetenga siku maalum ya ukusanyaji wa mapato ambayo wakuu wa idara hujigawa na wasaidizi wao na kwenda kukusanya mapato.”Alisema Dakawa.

Hatahivyo alitoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa kodi kwani wakifanikisha hilo watawezesha halmashauri kujiendesha yenyewe lakini pia itasaidia serikali kupata mapato na kujiendesha yenyewe bila kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili.

Wakuu wa Idara wakifuatilia kwa umakini baraza la madiwani kujadili taarifa za robo ya pili Oktoba hadi Desemba 2018

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *