Elimu

Kongwa wamkwaza Jafo, Atoa Maagizo Mazito kwa TAKUKURU

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb) amewaagiza Wakurugenzi kote nchini  wanaotekeleza miradi wa  kulipa kulingana na  matokeo  (EP4R)  kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Elimu  kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa asilimia mia ifikapo Februari, 2020

Ametoa maagizo hayo leo akati alipokuwa katika ziara ya kikazi ya  kukagua miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Jijini Dodoma.

 Jafo alisema Wakurugenzi wote watakaoshindwa kukamilisha miradi  hiyo kwa wakati  kuanaandika barua kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kueleza kushindwa kwao kutimiza majukumu  yao ya msingi ikiwepo hilo la  kukamilisha miradi hiyo kwa wakati  ifikapo tarehe 20, februari,2020

Waziri Jafo amemuelekza Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Bw. Gerald Mweli kuandaa taarifa  ya  wakurugenzi wote walioshindwa kukamilisha  ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia mradi wa EP4R na kuiwasilisha kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  ifikapo tarehe 20 Februari, 2020.

 Jafo amefafanua kuwa mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kuisoma atatoa mapendekezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta John Pombe Magufuli juu ya Wakurugenzi walioshindwa kutimiza wajibu wao.

“Miradi hii tunaijenga mahususi kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri, Serikali imetoa pesa ya kutekeleza miradi hii lakini kuna baadhi ya Wakurugenzi wameshindwa kusimamia utekelezaji wake ambapo fedha zimeisha lakini bado miradi haijakamilisha wakati katika maeneo mengine wametumia fedha hiyo hiyo na majengo yamekamilika kwa viwango,” amesema Mhe. Jafo.

Jafo  amewataka Wakuu wa Wilaya wote nchini ambapo Miradi ya EP4R inatakelezwa katika Halmashauri zao kuhakikisha wanawasimamia Wakurugenzi ambao wanalegalega katika kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na ifikapo tarehe 20 Februari, 2020 wawasilishe  taarifa kama Mkurugenzi wake ameshindwa kutekeleza majukumu yake

katika hatua nyingine amewaagiza Wakurugenzi  wote nchini  kuhakikisha wanasimamia  kwa weledi ujenzi wa miundombinu ya elimu  ili kuweza kukamilisha miradi  hiyo kwa wakati.

Akikagua ujenzi wa mabweni na bwalo katika shule ya Sekondari ya Kongwa,Mhe  Jafo amemtaka Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kongwa, Abdullah Urari  kuendelea kuchunguza chanzo cha miradi ya elimu kutokamilika huku fedha zilizotolewa zikiwa zimeisha.

“Sijaridhishwa na utekelezaji wa miradi katika sekta ya elimu,afya mnafanya vizuri,lakini elimu hapana,fedha hizi tulizoleta ndio tumepeleka kwa wenzenu wote,iweje hapa hali iwe tofauti,lazima kuna shida hapa.

Mhe. Jafo amewataka TAKUKURU kuchunguza  kama upande wa manunuzi kuna shida na kama kulikuwa na mianya ya ubadhilifu wa fedha za Serikali  ili wahusika wachukuliwe hatua  kwa kukwamisha  mradi huu.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU wilaya Bw. Abdullah Urari amesema tayari wameshaanza kufanya uchunguzi kuhusu mradi huo kwa maelelezo ya Mkuu wa Wilaya hiyo Deogratius Ndejembi aliyowahi kuyatoa.

“Tulichogundua katika uchunguzi wa awali hapa utaratibu wa manunuzi umekiukwa, “force account” haikufuatwa,walifanya makisio makubwa ya vitu na hivyo kupelekea vifaa  vingi kubaki na vitu vilinunuliwa kwa gharama kubwa,” amesema Urari.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi,Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kongwa Alex Salum alisema Januari mwaka huu walipokea kiasi cha sh milioni 290 toka wizara ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,mabweni mawili na bwalo la chakula.

Amesema mpaka sasa zaidi ya sh milioni 200 zimeshatumika ambapo ujenzi bado haujakamilika pamoja na kwamba baadhi ya vifaa vya kumalizia ujenzi huo vipo.

“Kwa sasa hapa ujenzi wa bwalo umefikia asilimia 75, ujenzi wa mabweni asilimia 95 na madarasa umefikia kwa asilimia 95,na matarajio yetu ni kukamilisha ujenzi huu ifikapo januari 15 mwakani,”alisema mkuu huyo.

Aidha katika ziara hiyo mbali na kutembelea ujenzi wa miradi hiyo katika shule ya Sekondari ya Kongwa,pia alikagua ujenzi wa maabara na mabweni katika shule ya Sekondari ya Sejeli na sekondari ya Ibwaga kabla ya kukagua ujenzi wa chumba cha upasuaji na maabara katika Hospitali ya wilaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *