Mafunzo

Ma DC na Ma DED Waaswa Kutatua Kero za Wananchi

Na Fred Kibano

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Wilaya (waliosimama), waliokaa kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Belinith Mahenge na Kaidari Singo Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Uongozi Tanzania, kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe na Dkt. Charles Mhina Mkurugenzi wa Serikali za Mitaaa Ofisi ya Rais TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kutatua kero za wananchi na kusimamia vema rasilimali za Serikali ili kuendana na dhamira ya Rais John Pombe Magufuli.

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya Wakurugenzi wapya wa Halmashauri na Wakuu wapya wa Wilaya yaliyokuwa yakifanyika Jijini Dodoma mapema wiki hii.

Waziri Jafo amewaagiza viongozi hao kutatua kero za wananchi kwa wakati na kuwa na ajenda ya Kudumu ya kuhakikisha wanatengeneza fursa za kiuchumi na ajira ili kuwainua kiuchumi vijana, akina mama na walemavu waliopo katika wilaya zao, lakini pia kuzingatia usafi na kuhakikisha wanapambana na Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya ambazo zinaathiri sana nguvu kazi ya vijana na hivyo waweke mikakati ya kuzuia na jinsi ya kupambana na janga hili.

Kuhusu rasilimali amewaagiza kwenda kubaini rasilimali mpya ambazo wengine walikuwa hawajaziona na kukakikisha zile zilizopo zinakuwa katika hali na matumizi mazuri na kuendelea kuwa hivyo kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa kuzisimamia na kuhakikisha hazitumiki vibaya. “Tumieni sheria, taratibu kanuni na bila kumnyanyasa yeyote kasimamieni rasilimali” alisema Jafo.

Aidha, Waziri Jafo amewaasa Viongozi hao kuzingatia mipaka ya kazi zao, nidhamu,kuepuka kufanya kazi kwa mazoea, kuwa na mahusiano mazuri baina yao na wananchi, kusimamia na kuhakikisha miundo mbinu inakuwa katika ubora unaotakiwa, usafi wa wilaya na halmashauri zao na kusimamia manunuzi mazuri na halali yenye manufaa kwa jamii kuanzia steji ya awali kabisa ya maombi.

Waziri Jafo alisema pia kuwa huduma bora za afya kwa wananchi zimeboreshwa kupitia Serikali ya Awamu ya tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Tanzania na tayari ameridhia kiasi cha fedha shilingi bilioni 333/= kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya 67 na ifikapo Novemba mwaka huu kila wilaya itapatiwa bilioni 1.5/= kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe ameowaonya viongozi hao juu ya matumizi mabaya ya madaraka kwani hupelekea wananchi kutafsiri kwamba hayo ndio maelekezo wapewayo.

“Ninawataka kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo inayotolewa na serikali katika nafasi zenu ambazo wananchi wanawaamini, ili mumtendee haki Rais pia.” Alisema Mhandisi Iyombe.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mheshimiwa Moses Joseph Machali mmoja kati ya Viongozi hao waliopatiwa mafunzo alitoa tamko la ahadi ya kuzingatia mafunzo hayo na kuishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Taasisi ya UONGOZI kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

 

Awali akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI Beatrice Kimoleta amesema mafunzo hayo ya siku nne yaliandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Tasisi ya UONGOZI na yalibeba mada tisa ambapo mada kuu ikiwa ni kusimamia Ulinzi, Usalama na Amani katika maeneo yao na hivyo zitawaongoza katika shughuli zao za Kiuongozi na kuleta mahusiano mazuri baina yao na wananchi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *