Habari za Wizara

Mabaraza ya Wafanyakazi Yaongeze Tija na Ufanisi Kazini – Kandege

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi zake kimefanyika hivi leo Jijini Dodoma ambao Mhe Kandege Naibu Waziri OR – TAMISEMI ametoa wito wa mabaraza ya wafanyakazi kuwa kiungo muhimu kati ya watumishi na Menejimenti

Na Fred Kibano

Serikali imetoa wito kwa watumishi wa Umma hapa nchini kuyatumia mabaraza ya wafanyakazi ili kuongeza ufanisi, maslahi na tija sehemu za kazi hali wakiwahudumia wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya na Miundombinu) Mhe Josephat Kandege kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika katika ofisi za OR – TAMISEMI Jijini Dodoma leo.

Mhe. Kandege amesema mabaraza hayo kupitia mikutano yake yaendelee kutoa tija katika maeneo ya kujadili malengo na mipango ya Wizara na Taasisi zake, maboresha ya utendaji kazi wa kila siku pamoja na kutetea maslahi ya Watumishi kwa ujumla.

“umuhimu wa baraza la wafanyakazi ni kutoa fursa kwa watumishi kupitia wawakilishi wao, kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine”

Aidha, Mhe. Kandege amesema Baraza la Wafanyakazi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwepo maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya Wafanyakazi na Uongozi wa Taasisi husika na kuhakikisha kunakuwepo na nidhamu ya kazi kwa madhumuni ya kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za Taasisi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema Uwepo wa Mabaraza ya Wafanyakazi pahala pa kazi msingi wake  ni  agizo la Mh. Rais  Na. 1 la mwaka 1970 na pia mchakato wa maandalizi ya bajeti ya OR-TAMISEMI umepitia katika hatua mbalimbali kwa watumishi kushiriki kikamilifu.

 

Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa katika kupanga bajeti za Mikoa na Mamlaka za  Serikali za Mitaa mwaka huu umetumika mfumo wa PLANREP ambao umesaidia kupunguza gharama katika maandalizi ya Bajeti  za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. 

Amesema tayari  bajeti hiyo imeshawasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa  na itajadiliwa katika kikao hiki cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara ili Watumishi wapate fursa ya  kufahamu nini kilichopangwa kutekelezwa katika mwaka wa  fedha 2019/2020 na kutoa michango ya  mawazo.

Kikao cha baraza hilo kilikuwa mahususi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na kujadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa maana ya taarifa ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/19, pamoja na bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *