Habari za mikoani

Madiwani Sumbawanga wajinoa suala la Mapato, Usafi, Njombe

Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakiwa kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe mara baada ya kuwasili kwa lengo la kujifunza maswala ya usafi wa mazingira na ukusanyaji mapato. (Aliyesimama) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminata Mwenda

Hyasinta Kissima- H/W Mji Njombe

Halmashauri ya Mji Njombe imepokea ugeni wa Waheshimiwa Madiwani wakiwa wameambatana na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga   lengo ikiwa ni kujifunza na kuongeza maarifa kuhusiana na masuala ya mapato na usafi wa Mazingira.

Haya yamebainika wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha wageni hao iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe, ambapo ugeni huo ulikiri wazi kuwa wamevutiwa kufika Halmashauri ya Mji Njombe kujifunza kutokana na sifa ambazo Halmashauri imekuwa ikijizolea kila mara katika eneo la usafi wa Mazingira pamoja na ukusanyaji mapato.

“Halmashauri ya Mji Sumbawanga kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tulikasimia kukusanya bilioni mbili na milioni mia tano, lakini hata hivyo hatukufanikiwa kukusanya asilimia 80 kwa mujibu wa maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu, na badala yake tulikusanya asilimia 54 pekee. Aidha kwa upande wa mashindano ya usafi na Mazingira tulishika nafasi ya pili kutoka mwisho kutokana na ukosefu wa vyoo bora na matumizi bora ya vyoo.”Alisema Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga. Justin Emmanuel Malisawa.

Alifafanua kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili ni kwenye utekelezaji wa sheria ndogo ndogo za Halmashauri na changamoto kutoka kwa wanasiasa ambao wamekuwa wakipinga na kutotekeleza ipasavyo baadhi ya maazimio waliyojiwekea kwenye ukusanyaji wa mapato na utunzaji Mazingira na ndio maana waliona umuhimu wa kuja kujifunza kutoka Njombe.

Akielezea mafanikio ya Halmashauri ya Mji Njombe ambayo imefikia kwa upande wa usafi wa Mazingira sambamba na ukusanyaji mapato, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi Illuminata Mwenda amesema kuwa mafanikio hayo yalitokana na utayari na kujitoa kwa Madiwani bila  kujali itikadi za vyama vyao na ushirikiano wa Wataalamu.

“Madiwani ndio wanaotaka Halmashauri yao iweje, hivyo ndivyo ninavyofahamu. Mnaweza mkawa na mipango mizuri lakini Waheshimiwa Madiwani wakisema hapana inakuwa sivyo.

Aliongeza kuwa Madiwani wao agenda zao kuu ni mapato na usafi. Na hata katika vikao vya wataalamu wamekuwa wakijadili na kuboresha mapungufu yanayojitokeza na kuweka mikakati thabiti kwenye ukusanyaji mapato na usafi wa Mazingira na tumekuwa tukifanikiwa kwa kiasi kikubwa.”Alisema Mwenda.

Dorcas Mkello ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Njombe alisema kuwa miongoni mwa mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia kwenye ukusanyaji mapato ni pamoja na utoaji wa motisha ya pikipiki kwa watendaji wanaofanya vizuri kwenye ukusanyaji mapato lakini pia  kuwapatia milioni 5 kwa kila Diwani kwa kila robo ya mwaka fedha ambazo hukabidhiwa kwa diwani wa  Kata husika kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwenye Kata yake. Kufuatia hali hiyo kila diwani amekuwa mlinzi kwenye usimamizi wa mapato kwani wasipofanya hivyo wanaelewa fika fedha hizo hazitapatikana bila kukusanywa kwa nguvu kubwa.

Kwa upande wake Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Lawi Bernard amesema kuwa licha ya kuwa na mwamko chanya wa wananchi kwenye uchangiaji wa tozo za taka, Halmashauri kupitia mapato ya ndani imekua ikiona umuhimu wa kuiwezesha idara hiyo na ndio maana kwa mwaka wa fedha 2018/2019 walifanikiwa kutenga fedha kupitia mapato ya ndani na kununua tractor kwa ajili ya kubeba taka na hivyo kuzuia mlundikano wa taka katika maeneo ya Mji kutokana na uwepo wa vitendea kazi vya kutosha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga alisema kuwa, siri ya mafanikio ni umoja baina ya Waheshimiwa Madiwani na wataalamu kwani wamekuwa wakipokea maelekezo ya wataalamu na panapokuwa na mapungufu wamekuwa wakishirikiana kuboresha kwa manufaa ya Halmashauri nzima.

“Wenzangu wa Sumbawanga niwaombe muwe na ushirikiano katika ukusanyaji mapato. Maendeleo ni ya wananchi wote na hayana vyama, naomba pia mfahamu kuwa katika swala la Usafi na Mazingira hamtaweza kufanya vizuri kwa kutegemea Halmashauri itaondoa taka yenyewe, lazima mzalisha taka awe na jukumu la kuondoa taka kwa kuchangia gharama.”Alisema Mwanzinga.

Aidha, Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga wameishukuru Halmashauri ya Mji Njombe kwa elimu waliyoipata na wamepongeza ujenzi wa kiwango cha hali ya juu unaoendelea  katika kituo kipya cha Mabasi na wameahidi kutengeneza mtandao wa mawasiliano na Halmashauri ya Mji Njombe ili kuendelea kupata ujuzi na mbinu mpya katika maeneo mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Mji Njombe kwa miaka miwili mfululizo; 2017/2018 na 2018/2019 imepokea wageni kutoka Halmashauri nane za Mikoa ya Songwe, Singida, Shinyanga na Rukwa kwaajili ya kujifunza mbinu na siri ya ushindi inayotumia Halmashauri ya Mji   Njombe katika kuimarisha hali ya usafi katika maeneo yake yote.

Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Dorcas Mkello akiwasilisha mada ya ukusanyaji mapato kwa Wahe. Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga
Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Lawi Bernard, akitoa mpango mkakati wa Halmashauri ya Mji Njombe wa utunzaji na uthibiti wa taka ngumu kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya mafunzo ya timu hiyo katika Halmashauri ya Mji Njombe.

 

Afisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Isack Mapunda akitoa ufafanuzi wa matumizi bora ya mashine za ukusanyaji mapato (POS) kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka katika Manispaa ya Sumbawanga wakati wa ziara ya mafunzo ya timu hiyo katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi unaofadhiliwa na benki ya dunia kupitia mradi wa uboreshaji na uimarishaji Miji (ULGSP) katika Halmashauri ya Mji Njombe ni miongoni mwa mradi uliotembelewa na Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu kutoka Manispaa ya Sumbawanga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *