Habari za Kiuchumi/Kilimo

Makatibu Tawala Mikoa simamieni Matumizi na Manunuzi ya Umma katika Halmashauri

Na Fred Kibano

Serikali imewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa na kusema itaendelea kuimarisha hali ya ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Umma kwenye halmashauri nchini ili kuinua uchumi wa mamlaka husika na kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Kauli hiyo ameitoa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha maboresho ya fedha katika halmashauri nchini ambapo amewataka Makatibu Tawala kusimamia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri samabamba na matumizi ya fedha za Umma.

“tumewaita Makatibu Tawala wa Mikoa ili kuweza kuboresha hali ya masuala ya fedha katika mikoa na halmashauri zao ikiwa ni pamoja na mipango ya mikoa, vitu muhimu ni vya msisitizo ni matumizi ya fedha za Umma kuanzia fedha za makusanyo katika vyanzo vya halmashauri, kutoka Serikali Kuu na fedha za Wadau wa Maendeleo kwamba zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa”

Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa suala la kuimarisha Vitengo vya ukaguzi vya ndani limetiliwa mkazo ili kuweza kubaini ubadhilifu katika hatua za awali na pia kuimarisha Vitengo vya manunuzi ili kuona sheria, kanuni na taratibu za mwaka 2016 za manunuzi ya Umma zinafuatwa na kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI itafanya ukaguzi ili kubaini kama kuna ubadhilifu na ukiukwaji wa matumizi ya fedha za Umma.

Kwa upande wake Shomari Mukhandi Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usimamizi wa Fedha Ofisi ya Rais TAMISEMI akitoa taarifa ya jumla ya mradi katika kikao tendaji cha mradi amesema kwa hivi sasa awamu ya tano inayokuja itahusisha mikoa yota ikiwa na malengo ya usimamizi wa matokeo mazuri ya fedha kwa kupata hati safi na kuboresha mapato ya halmashauri nchini.

“programu hii imechangia maboresho ya hali ya fedha katika hamashauri nchini ambapo asilimia 90 zisizo na mashaka zimeongezeka ikilinganishwa na asilimia sitini za hapo awali, aidha umewezesha kupanga na kusimamia mapato ya halmashauri kwani ongezeko la maptao ni asilimia 80 ya mipango yao ikilinganishwa na hapo awali”  

Naye Magreth Chipeta Afisa wa Serikali za Mitaa mkoa wa Rukwa amesema kimsingi  programu hii ya maboresho ya mfumo wa fedha imesaidia sana mkoa wa Rukwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ukilinganisha na ukusanyaji mdogo wa hapo awali ambapo imeongeza mapato kwa asilimia 30.

“awali mkoa wa Rukwa ulikuwa ukikusanya shilingi bilioni 2.1 mwaka 2012/2013 lakini mwaka 2017/2018 mfumo wa kielektroniki umesaidia kukusanya shilingi bilioni 6.9 sawa na ongezeko la asilimia 30, kwa mfano manispaa ya Rukwa pekee imekusanya asilimia 97 ya lengo walilojiwekea na Nkasi asilimia 82”

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga akifungua kikao kazi kilichohusisha Makatibu Tawala wa Mikoa, Wataalam wa Fedha na Wadau wa Maendeleo katika kikao kazi cha maboresho ya mfumo wa fedha katika mikoa na halmashauri nchini Jijini Dodoma leo.

Aidha, Bi. Chipeta mfumo umesaidia kuondoa hoja za kutoka hoja 536 awali hadi hoja 282 kwa hivi sasa, mfumo pia umesaidia kutoa mafunzo kwa madiwani, watumishi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa na ofisi za halmashauri za wilaya mkoani Rukwa.   

Maboresho ya Programu ya Fedha (Public Financial Management Reform Programme – PFMRP) ilianzishwa hapa nchini katika mwaka wa fedha 2014/2015 na kukamilika mwaka 2016/2017 kwa lengo la kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato na matumizi mazuri ya fedha za Umma ili kutoa huduma bora na kuleta maendeleo katika mikoa kumi ya Dodoma, Geita, Katavi, Mara, Simiyu, Mtwara, Njombe, Kigoma, Rukwa na Ruvuma ambayo ilikuwa nyuma kimapato.

Hivi sasa mfumo huu upo katika awamu ya tano na itakuwa ya miaka mitano kuanzia 2017/2018 hadi 2021/2022 na itahusisha mikoa yote ishirini na sita na unalenga uwazi, uwajibikaji, ufanisi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za Umma.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *