Habari za Wizara

Mawasiliano yarejeshwa kwa Wananchi wa Chinangali II na Mlebe

Nteghenjwa Hosseah, Chamwino.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (kwanza kulia), Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Vumilia Nyamwaga(katikati), Meneja wa TARURA Wilaya ya Chamwino Nelson Maganga wakati wa ziara yake ya kukagua daraja la mlebe na barabara ya Chinangali II – Mlebe- Mnase na Mgunga yenye urefu wa Km 22.8.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (kwanza kulia) akipokea taarifa ya ujenzi wa daraja la mlebe toka kwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Chamwino Eng. Nelson Maganga(kwanza kushoto).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (kulia) akiteta jambo na Meneja wa TARURA Wilaya ya Chamwino Eng. Nelson Maganga.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (kwanza kulia) akipokea maelezo toka wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Chamwino Eng. Nelson Maganga baada ya kupima upana wa barabara za lami zinazojengwa Chamwino Mjini.
Muonekano wa barabara zinazondelea kujengwa kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Km 3.5 Chamwino mjini.

Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wamefanikisha kujenga daraja lililoharibiwa vibaya na mvua za masika na kupelekea kukatika kwa mawasiliano baina ya kijiji cha Chinangali II kilichopo Kata ya Buigiri na kijiji cha Mlebe kata ya Msamalo Wilayani Chamwino.
Akitembelea daraja hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amepongeza upngozi wa TARURA kwa kurejesha mawasiliano baina ya vijiji hivyo kwa kujenga daraja la mlebe sambamba na kujenga barabara ya Chinangali II – Mlebe – Mnase – Mgunga.
Akizungumza katika ziara ya kukagua barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua katika Wilaya ya Chamwino mapema leo hii Waziri Jafo amesema liona malalamiko ya wananchi wa Chamwino kupitia mitandao ya kijamii na nikayawasilisha kwa uongozi wa TARURA na kuwaagiza kuchukua hatua stahiki na leo hii nimekuja kuthibitisha utekelezaji wa maelekzo yangu.
“Nafurahi kuona mawasiliano yamerejeshwa na sasa vijiji vya Chinangali II na Mlebe vinaweza kuwasiliana na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kujitaftia kipato huku wakizifikia huduma za Afya na Elimu kwa urahisi zaidi” alisema Mhe. Jafo.
Waziri Jafo aliongoza kuwa hivi ndio Serikali inavyotakiwa kufanya kazi ukiiagiza Taasisi kutatua changamoto zinazowakwaza wananchi wanatatua kwa wakati na kurejesha huduma stahiki na wakati wote napenda namna TARURA wanavyofanya kazi zao ni za viwango na zinazokithi mahitaji hongereni sana.

Katika ziara hiyo pia Waziri Jafo alikagua barabara za lami zinazoendelea kujengwa Chamwino Mjini zenye urefu wa Km 3.5 na kusisitiza TARURA kuendelea kusimamia ubora katika ujenzi wa barabara hizo.
“Simamieni Wakandarasi kwa makini katika ujenzi wa barabara hizikwa sababu zinagharimu fedha nyingi sana hizi km 3.5 zinazojengwa hapa ni zaidi Tsh. Bil 1.5 ili vile vipimo vinavyotakiwa kwenye barabara vipatikane kama Tabaka la Chini, la kati mpaka lile la juu pia muhakiki upana wa barabara unaotakiwa unafikiwa kwa vipimo vyenu na sio vya mkandarasi” alisema Mhe. Jafo.
Akizungumzia ujenzi wa daraja sambamba na barabara iliyoharibiwa na mvua Meneja wa TARURA Wilaya ya Chamwino Eng. Nelson Maganga anasema kuwa kupitia mfuko wa barabara walitenga Tsh Mil 41.9 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na daraja la mlebe lakini mkandarasi aliyepatikana atajenga kwa gharama ya Tsh Mil 37.5 hivyo kuna bakaa ambayo itatumika kuendelea kuimarisha barabara zingine zilizoathirika.
“Pamoja na juhudi kubwa za Serikali katika kutatua changamoto za barabara hii wananchi wa Mlebe walianza kujitolea kwa kukusanya mawe na kuponda kokoto kwa lengo la kurekebisha eneo hilo lakini TARURA Chamwino Dc iliwapongeza na kuwashukuru wananchi wa kijiji cha mlebe kwa jitihada zao kisha TARURA kuendelea kujenga barabara pamoja na daraja hilo” alisema Eng. Maganga.
Kwa hivi sasa barabara ya Chinangali II – Mlebe – Mnase – Mgunga yenye urefu wa Km 22.8 pamoja na madaraja kwa sasa inapitika vizuri kutokana na matengenezo mazuri yaliyofanywa na TARURA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *