Habari za mikoani

Mbunge Sanda Awacharukia Wakandarasi wanao suasua Miradi wa Maji

Mh. Edwin Sannda akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa mafundi waliojenga kituo cha maji ikiwa ni moja ya miradi inayoendelea kujengwa Kondoa Mjini

Na Sekela Mwasubila- H/W Kondoa

Wakandarasi wanaotekeleza kazi ya kusambaza miundombinu ya maji katika Halmashauri ya Mji Kondoa wametakiwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.

Hayo yalibainishwa na Mbunge wa Kondoa Mh. Edwin Sanda wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji aliyoifanya hivi karibuni ili kujiridhisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kuwa wakandarasi hao walipewa miezi sita ya kufanya kazi lakini kwa uhalisia kazi hiyo haihitaji miezi hiyo sita kwani hadi kipindi hicho cha miezi mitatu waliyokwishafanya kazi wengi wapo katika hatua nzuri isipokuwa mkandarasi mmoja.

“Natamani kazi hii ingekamilika chini ya miezi minne ili wananchi waanze kupata huduma ya maji lakini pia itawapunguzia gharama za mradi kwani kazi inapochukua muda mrefu hata gharama za uendeshaji huongezeka na kuwa hasara kwa mkandarasi”alisema Sanda.

Hata hivyo aliwapongeza wakandarasi watatu waliofanyakazi kwa asilimia zaidi ya sabini kwa kukamilisha ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, vituo vya kuchotea maji, ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji na utandazaji wa mabomba ambapo wamehaidi kukabidhi mradi mwishoni mwa mwezi Februari.

Aidha Mh. Sanda alisikitishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Hospitali ya wilaya na kumuagiza Mkurugenzi wa Mji kuwaita viongozi wa kampuni hiyo kuelezea sababu za kusuasua hali ambayo inaweza kusababisha mradi kutokamilika kwa wakati na kuwakosesha huduma ya maji wananchi.

Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji inatekelezwa Halmashauri ya Mji Kondoa ambapo serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya usambazaji wa miundombinu hiyo katika visima vitano kati ya kumi vilivyochimbwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni miatano.

Mbunge wa Kondoa Mjini Mh. Edwin Sannda akiwa katika moja ya vioski vya kuchotea maji katika moja ya mradi wa usambazaji wa miundombinu ya Maji Kondoa Mjini
Mbunge Mh. Edwin Sannda akipanda juu ya moja ya matanki ya kuhifadhia maji katika ujenzi wa miradi ya maji inayoendelea Kondoa Mjini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *