Mafunzo

Mfumo wa Epicor 10.2 Kudhibiti Upotevu wa Mapato ya Serikali

 

Wataalam wa fedha waliohudhuria mafunzo ya mfumo wa fedha ‘epicor 10.2 kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Ruvuma na Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mradi wa Uimarishaji Mifumo Umma (Public Sector Systems Strengthening – PS3) chini ya Shirika USAID.

Na. Fred Kibano

Mafunzo ya mfumo wa fedha wa kielektroniki wa Epicor 10.2 yanaendelea nchini kote kwa kada za wahasibu na waweka hazina, maafisa ugavi na wataalam wa mifumo ya fedha yanayolenga kuwajengea uwezo wataalam hao kukusanyia mapato na kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.

Mafunzo haya yanafanywa baina ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mradi wa Uimarishaji Mifumo Umma (Public Sector Systems Strengthening – PS3) chini ya Shirika USAID lengo likiwa ni kuziimarishia halmashauri mifumo ya ufuatiliaji fedha ‘Epicor accounting systems’ ili kuboresha usimamizi wa fedha, kusimamia matumizi ya fedha na utoaji wa huduma bora za kifedha.

Suzana Chaula mhasibu wa Halmashauri ya Mji Kibaha anasema maboresho yaliyofanywa yatasaidia katika kutoa taarifa za hesabu za Serikali kwa maana ya ufungaji wa hesabu za kila mwezi na mwisho wa mwaka, ikiwa ni pamoja na kupunguza hoja za ukaguzi.

 “mfumo utasaidia utoaji wa taarifa za kihesabu kwa kudhibiti matumizi na kujua nini kinaendelea katika baeti na matumizi lakini pia ufanyaji wa tathmini kama umefikia malengo”

Suzana Chaula anabainisha kuwa mfumo wa epicor 10.2 hauwezi kuwa mzuri bila ya watumiaji kujengewa uwezo, hivyo Serikali imefanya vema kuuimarisha mfumo huu wa fedha ili kuondoa hoja za ukaguzi.

“katika mfumo wa mapato tunaamini kuwa kuanzia mwezi julai, utatatua changamoto zinazotokana na hoja za ukaguzi kwani utatoa taarifa upande mmoja kwenda mwingine kwani mifumo itakuwa inaongea pamoja”

Ummy Wayayu Mhasibu Mwandamizi kutoka kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, anasema kwamba maboresho yaliyofanywa katika epicor 9.05 na kupata mfumo wa 10.2 yatasaidia kuondoa kabisa changamoto za fedha zinazotokana na mfumo epicor 9.05, kwa kuwa mifumo yote sasa itakuwa na mawasilino ya moja kwa moja kama vile epicor 10.2 kurahisishia ufanyaji kazi wa mifumo ya planrep, bajeti na FFARS.

Dkt. Gemini Matei kiongozi wa timu ya Mradi wa PS3 anasema mfumo wa epicor 10.2 utakuwa na manufaa makubwa mbali na kusaidia uandaaji wa taarifa za fedha za mwaka, utaunganisha mifumu mingine.

“huu mfumo wa Epicor, zaidi ya kuboresha kazi za kila siku, utawezesha kuunganishwa mfumo wa Planrep, mfumo wa FFARS  pamoja na mifumo mingine lakini pia utarahisisha kuandaa ripoti ya fedha ya mwaka”

Serikali imekuwa ikitumia mifumo kadhaa kwa kukusanyia mapato na mpaka sasa mfumo wa Epicor 9.05 unatumika katika halmashauri 151 na epicor 10.2 umeanza kutumika kwenye halmashauri 34 na kusudio ni mamlaka zote zianze kutumia epicor 10.2 iliyoboreshwa.

Mifumo mingine ya fedha inayotumiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ni Mfumo wa Mipango, Bajeti na Taarifa za fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (Local Government Planning, Budgeting and Reporting Systems – Planrep) uliopo katika hamashauri zote 185, Mfumo wa Ufuatiliaji na kutolea taarifa za fedha (Facility Financial Accounting and Reporting System – FFARS), Mfumo wa Usimamizi Taarifa za Hospitali (Hospital Management Information System ‘GoT-HoMIS’, Mfumo wa Ukusanyaji mapato na kutoa taarifa katika halmashauri (Local Government Revenue Collection Information Systems – LGRCIS) ambayo inatumika serikalini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *