Habari za Wizara

Mhe. Magufuli awashukuru wadau wa maendeleo wa mfuko wa pamoja wa afya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akiwa na wadau wa mfuko wa pamoja wa afya, wakikata utepe wakati kufungua Kituo cha Afya cha Madaba, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma.

Na. Angela Msimbira  RUVUMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Afya Nchini kwa kujitoa kwa hali na mali katika kusaidia kufanikisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya nchini

Ameyasema hayo leo wakati akifungua kituo cha afya cha Madaba kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma, moja ya vito 352 vilivyojengwa kupitia wadau wa maendeleo wa  sekta ya afya  nchini.

Mhe. Magufuli amewashukuru wadau hao kwa mchango mkubwa katika    ufanikisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchini jambo ambalo limeleta mabadiliko na kupunguza changamoto zilizokuwa zinaikabili  sekta ya afya nchini.

Mhe. Magufuli amefafanua kuwa sekta ya afya ni muhimu katika maendeleo ya taifa kwani watu wasio na afya njema ni ghrama kubwa kwa taifa na hudumaza maendeleo ya nchi, hivyo serikali imeamua kuwekeza katika Sekta ya afya ili kuwa na wananchi wenye afya bora ili kufikia uchumi wa kati..

“Ripoti ya shirika la afya duniani inaonyesha kuwa nguvu kazi iliyopotea kwa sababu ya magonjwa barani Afrika ni sawa na saa milioni 630 na inaonyesha kuwa endapo nchi za Afrika zitashindwa kuwekeza vizuri kwenye masuala ya afya zitapoteza wastani wa dola za kimerikani trioni 2.24 kwa mwaka hiki ni kiasi kikubwa sana  cha upotevu wa muda hivyo  kulitambua hilo  Serikali iliamua  kuwekeza kikamilifu katika sekta ya afya”Amesema Mhe. Magufuli.

Ameendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya afya ili kuweza kuwasaidia wananchi wa hali ya chini ambao wanachangamoto kubwa katika kupata huduma karibu na maeneo yao.

Mhe. Magufuli amesema Serikali kwa sasa imebadilisha utaratibu wa kuhakikisha fedha zote za ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchini zinapelekwa moja kwa moja kwenye vituo husika ili ziweze kutumika kwa malengo yalioyopangwa na kuleta mabadiliko katika vituo hivyo.

Aidha amewapongeza wananchi na uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuhakikisha wanasimamia kwa umakini mkubwa ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, jambo ambalo limesaidia vituo hivyo kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.

Wakati huohuo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Senkamba Kandege amewashukuru wadau  wa Mfuko wa afya wa pamoja (Basket Fund), wananchi na watumishi wa Serikali za Mitaa kwa kujitoa kwao katika  kufanikisha utekelezai  wa mikakati wa maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini.

Mhe. Kandege amesema kituo cha Afya cha Madaba ni miongoni mwa vituo vya kutolea Huduma za Afya 352 ambavyo vimekarabatiwa na kujengwa kupitia mpango wa maboresho wa afya msingi nchini

Amefafanua kuwa Kituo cha Madaba kimejengwa kwa gharama shilingi milioni 665 ambapo shilingi milioni 220 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba, milioni 445 zilitumika  katika ujenzi wa kituo hicho.

Ameleeza mchanganuo wa fedha hizo na kusema kuwa  shilingi milioni 400 zimetoka katika mfuko wa afya wa pamoja,  shilingi milioni 7.2  ni nguvu za wananchi wa Madaba  na  shilingi milioni 38.3  ni kutoka makusanyo ya  ndani ya Halmashauri  ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma.

Aidha Mhe. Kandege amesema kuwa OR-TAMISEMI imeweka mikakati ya kuboresha huduma za afya  kuanzia ngazi ya msingi kwa kukarabati miundombinu  katika vituo vya afya 535 nchini ifikapo mwaka 2020 ambapo mpaka sasa  vituo 304 vimekamilika lengo ni kuhakikisha maboma  1885 yaliyojengwa kwa nguvu za Wananchi yanakamilika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akiwa na wadau wa mfuko wa pamoja wa afya, wakikata utepe wakati kufungua Kituo cha Afya cha Madaba, kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe, Josephat Senkamba Kandege wakati wa kufungua kituo cha Afya Madaba kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *