Habari za mikoani

Mhe. Mongella asisitiza ukusanyaji wa Mapato kwa kutumia Mfumo wa kielektoniki

Na Remija Salvatory

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella ameongoza kikao cha Ushauri cha Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kujumuisha wajumbe mbalimbali wa kikao hicho ikiwa ni pamoja na Mhe.Waziri wa Kilimo Mifugo  na Uvuvi Mhe. Dkt.Charles, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo na Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula, Waheshimiwa Wabunge,Wakuu wa Wilaya,wakurugenzi,Meya wenyeviti na baadhi ya walikwa kutoka Taasisi mbalimbali.

Mhe. Mongella pamoja na kutoa Maagizo mbalimbali kwa watendaji kuhusiana na hoja zilizojitokeza kutoka kwa wajumbe wa Kikao hicho ,alisisitiza kuhusiana na  Makusanyo ya Mapato ya Ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na Matumizi ya Mfumo wa Kieletroniki (LGRCIS),’’Halmashauri yoyote isiyotumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya ndani inakiuka taratibu na sheria na ikibainika itachukuliwa hatua za kisheria ”.

 

Akiwasilisha Taarifa ya  Makusanyo ya Mapato ya Ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Afisa Usimamizi Fedha wa Mkoa  Charles Julius Misango  ameeleza kuwa Halmashauri za Mkoa wa Mwanza zilijiwekea malengo ya kukusanya jumla ya TZS 35,552,216,000.00 na Jumla ya TZS 9,812,583,537.17  sawa na 28% ya lengo zimekusanywa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2017 ambapo kwa kipindi cha Julai-Novemba cha Mwaka 2017/2018 makusanyo halisi ya Mapato ya Ndani yameongezeka kwa asilimia 3.2 (9,812,583,537.17 kutoka 9,507,901,255.23) ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha Julai–Novemba cha mwaka wa fedha uliopita 2016/2017.

Misango ameongeza kuwa,ongezeko hili la 3.2% si haba, hasa ukizingatia uchukuliwaji wa vyanzo vikubwa vya mapato kama vile kodi za majengo, Bill boards kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwenda Serikali Kuu (TRA),pia Mfumuko  wa  bei   umedhibitiwa   na    umeendelea kubakia katika wigo wa   tarakimu moja (Current Inflation rate is   5% as per August,2017).

Aidha, Mfumo wa kieletroniki wa Makusanyo ya Mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (local Government Revenue Collection System-LGRCIS), ulianzishwa na unasisitizwa utumike kwasababu kuu ya kuwezesha ukusanyaji wa Mapato na taarifa kwa vyanzo vyote mapato  vinavyopaswa kukusanywa kisheria na Mamlaka za Serikali za Mitaa,kuhifadhi kumbukumbu za walipa kodi na kutoa hati za madai (ankara) stakabadhi (risiti) kwa walipa kodi, ushuru na tozo mbalimbali kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa,kusimamia Ukusanyaji wa Mapato kwa urahisi zaidi na Utunzaji wa Kumbukumbu za walipa kodi kwa maana ya watu, wafanyabiashara wadogowadogo na makampuni.

Hata hivyo,Mfumo wa mapato unasaidia kufanya usuluhishi wa taarifa za mapato ya fedha zilizokusanywa.Makusanyo yaliyokusanywa kwa mwaka husika yanasidia sana katika kufanya tathmini na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka Makadirio sahihi na Malengo katika Mipango yao kwa miaka inayofuata ikiwa ni pamoja na  kurahisisha Uhakiki na Ukaguzi wa fedha za Umma kwani unazuia udanganyifu unaoweza kujitokeza kwa watumishi  wasio waaminifu.Mfumo huu wa ukusanyaji wa mapato (LGRCIS) unasaidia upatikanaji wa taarifa na ripoti mbalimbali kwa haraka na pindi tu zinapohitajika ikiwa ni pamoja na kuongeza dirisha la upatikanaji wa taarifa kwa ngazi ya Taifa na kutoa taarifa za kina za vyanzo vya mapato,kudhibiti Mianya ya rushwa na mapato ya Halmashauri  na pia Kutumika kama chanzo cha Mipango na Bajeti za Maendeleo kupitia taarifa  mbalimbali zinazotolewa pia malipo kwa njia ya kieletroniki yameongeza uwazi na usalama wa fedha zinazokusanywa na Mfumo huu wa Mapato (LGRCIS).

Misango ameongeza kuwa, Mfumo huu unarahisisha na kuongeza wigo wa ulipaji kodi kwa wananchi kwa kuwezesha njia mbalimbali za kieletroniki za ulipaji wa miamala ya kifedha, ikiwa ni pamoja na kupitia mifumo mbalimbali ya kibenki na huduma za kifedha za makampuni ya simu za kiganjani pia Mlipa kodi kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji na kutumia muda mfupi katika ulipaji na kupewa stakabadhi yake papo hapo bila tena kuhitajika kurudi kwa mlipaji (cashier) wa Halmashauri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *