Habari Kitaifa

Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA ya OR-TAMISEMI Yamkosha Katibu Mkuu OWM Prof. Kamuzora

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Fausine Kamuzora, akipata Maelezo kutoka kwa Mtaalam wa TEHAMA wa OR-TAMISEMI, Antidius Anatory, wakati wa Ziara ya Kikazi katika Ofisi hiyo, jinsi Komputa Kuu inavyofanyakazi.
Mtaalam wa TEHAMA,  Melkiory Baltazary  Akifanya Mawasilisho kwa Katibu Mkuu kuhusu Mfumo wa GoTHoMis, wakati wa kikao hicho.

Na Atley Kuni TAMISEMI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu Prof. Faustin Kamuzora, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusema ni kazi nzuri inayopaswa kuungwa mkono na kila mdau huku akitoa ahadi ya kuisemea mifumo na miundombinu OR-TAMISEMI pindi atakapo pata fursa ya kusema.

Prof. Kamuzora ameyasema hayo baada ya kufanya kikao kazi baina yake na watendaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kupitia Idara ya TEHAMA kufuatia mawasilisho kadhaa kuhusu mifumo inayoendeshwa na Ofisi hiyo.

“Huko nje wenzenu tukisikia Local Government, mawazo yetu tulio wengi tunafikiri mambo yapo ki-local local lakini kumbe hali ni tofauti kabisa” alisema Prof. Kamuzora.

Prof. Kamuzora mara baada ya mawasilsho ya mifumo hiyo kutoka kwa wataalam mbalimbali wa Idara TEHAMA, amewataka OR-TAMISEMI kuwatumia Wataalam wa Sheria wa Ofisi hiyo ili mifumo iliyobuniwa na kusanifiwa na OR-TAMISEMI  iweze  kupata hati miliki (copyright and property right).

Prof. Kamuzora pia, ametoa rai ya kutambuliwa kwa wataalam waliojitoa kwa moyo wa kizalendo hadi kukamilisha kazi hizo ambazo zimekuwa na tija kwa taifa, “ni vema sasa kuwatambua wataalam wanaotengeneza na kusimamia mifumo ya TEHAMA ili kuongeza motisha na ubunifu’’ amenukuliwa Prof. Kamuzora.

Sambamba na kuwatambua wataalam hao, Prof. Kamuzora amewaasa wataalam hao kuhakikisha kuwa kuna utaratibu wa kutambua vyanzo vya mapato ya ndani ya MSM ambavyo vimehamishwa kwenye Mamlaka zingine kama TRA ili takwimu zake zinaendelee kubaki katika mfumo wa LGRCIS kwa ajili ya kupima ufanisi wa chanzo husika ki-Halmashauri.

Aidha, Prof. Kamuzora amesisitiza uwepo na mfumo wa pamoja wa utoaji taarifa na takwimu (National Statistical System) kati ya taasisi za Serikali (mfano, RITA, NIDA, OR-TAMISEMI na NBS) ili kuepukana na kutofautiana kwa taarifa na  takwimu.

Wakati huo huo Katibu Mkuu OWM, ameonesha dhamira ya dhati ya kuunganishwa kwa mifumo ya TEHAMA na Takwimu katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma huku  akitaka ushirikiano na wataalam wa OR-TAMISEMI katika ujenzi na maboresho mbalimbali ya TEHAMA na takwimu ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA TAMISEMI, Bw. Baltazari Kibola, alimshukuru Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hatua ya kutembelea OR-TAMISEMI ili kujifunza kuhusu mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayosimamiwa na OR-TAMISEMI, huku akiahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.

“Ndugu Katibu Mkuu, kwa niaba ya Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, tunaahidi kufanyia kazi maelekezo yote ambayo umetupatia” alisema Kibola na kuongeza “lakini pia tunakuahidi utayari wetu wa kufanya kazi bila kuchoka kwa manufaa ya watanzania wote”.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Obey Assey, aliyekuwa ameambatana na KMOWM alipongeza jitihada mbalimbali za wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali, hasa Mradi wa PS3 unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Marekani, USAID ambao wanashirikiana na Serikali kuimarisha wa mifumo TEHAMA ya Umma.

Akiongea pembeni ya kikao kazi hicho Assey alisema, “Kuna baadhi ya watu hawajui PS3, lakini kumbe kazi yao wanayoifanya kwa kushirikiana na Serikali ni kubwa katika uimarishaji wa mifumo”.

Wakati wa mawasilisho ya mifumo, Katibu Mkuu – OWM alijionea jinsi  mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za Elimumsingi (BEMIS); Mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) wa  LGRCIS;  Mfumo wa Uandaaji wa Mipango na Bajeti za MSM ulioboreshwa (PlanRep); Mfumo wa Uhasibu wa utoaji taarifa za fedha katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma (FFARS); Mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya (GoT-HoMIS); Mfumo shirikishi wa malipo ya fedha za Umma (IFMIS-Epicor), Mfumo wa Tovuti (GWF) pamoja na Muungano Gateway ambayo iliwasilishwa na wataalam mbalimbali kutoka  Idara ya TEHAMA ya OR-TAMISEMI.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA, OR-TAMISEMI Baltazari-Kibola akitoa Maelezo ya awali mbele ya Katibu Mkuu OWM anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Faustine Kamuzora na Ujumbe wake wakati wa kikao kazi hicho.

 

James Mtitifikolo, Mtaalam wa TEHAMA, hapa akifanya uwasilishwaji wa Mfumo wa PlanRep kwa KM-OWM, katika Ukumbi wa Mikutano wa OR TAMISEMI katika Jengo la Sokoine.

 

Jinsi Miundo Mbinu ya TEHAMA ilivyo sambaa Nchini.
Mtaalam wa Takwimu kutoka Ofisi ya Raid TAMISEMI,  Iman Kaseki akiwasilisha juu ya Mfumo wa BEMIS jinsi unavyo fanyakazi wakati wa Kikao hicho na KM-OWM Prof.-Faustine Kamuzora.
Dkt.-Boniface-Kutoka-TAMISEMI-akifafanua-jambo-wakati-wa-kikao-hicho-na-KM-OWM-Sera-na-Uratibu
Antidius Anatory Mtaalam wa TEHAMA, akifanya wasilisho la Mfumo wa Mapato wa LGRCIS.
Mtaalam wa Habari Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Atley Kuni, akifanya Mawasilisho ya mada ya Mfumo wa Tovuti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (GWF), katika kikao hicho.
Timu ya wataala wa TAMISEMI wakiwa wanafatilia kwa umakini wakati wa kikao hicho.
Timu iliyo ambatana na Prof. Faustine Kamuzora, Katibu Mkuu OWM, ikiwa inafanya ufatiliaji wa kina wakati kikao hicho.