Elimu

Msiwaadhibu Walimu kwa Matokeo Mabaya ya Wanafunzi – Nzunda

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda akitoa maagizo ya Serikalikwa Viongozi wa Elimu mkoani Kigoma. Kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma Rashid Mchata na kushoto ni Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma Juma Kaponda 

Na Fred Kibano

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda amewataka Viongozi katika Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingine zinazohusika na walimu kutowaadhibu walimu kutokana na matokeo mabaya ya mitihani ya mwisho.

Nzunda ametoa kauli hiyo hapo jana wakati wa kikao kazi alichofanya mjini Kigoma na Maafisa Elimu Wilaya Msingi na Sekondari, Maafisa Elimu Taaluma Msingi na Sekondari, Maafisa Vielelezo na Takwimu Msingi na Sekondari, Waratibu Elimu Kata, Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari, baadhi ya walimu wa msingi na sekondari na Wathibiti Ubora wa Elimu kwa lengo la kutoa maagizo ya Serikali kwa mkoa huo na mikoa mingine nchini ili kuendelea kuboresha elimu mashuleni.  

“Viongozi katika Sekta ya Elimu wasifanye kazi ya kuwaadhibu Walimu, Waratibu wa Elimu Kata kwa sababu tu ya wanafunzi kufeli mtihani wa mwisho wa kidato cha nne, kidato cha sita au mtihani wa kuhitimu darasa la saba, kwa sababu inawezekana watoto wamefeli si kwa sababu yenu ni kwa sababu ya watoto wenyewe, ila tuwaadhibu walimu kwa sababu ya kushindwa kutoa taaluma, utoro madarasani, utoro shuleni, kutokuzingatia taratibu za ufundishaji na ujifunzaji, suala la maadili, hilo ndilo liwe sababu kama kuna haja ya kufanya hivyo”

Amesema matokeo ya mtihani wa mwisho yawe ni kipimo cha kujitathmini, kujipanga upya na kujisahihisha kwani wakifanya hivyo itakuwa rahisi kuimarisha taaluma nchini katika ngazi zote.

Aidha, amekemea tabia ya wizi na uvujaji wa mitihani na utoaji wa rushwa na kwamba mtumishi wa Umma atakayebainika ataondolewa katika utumishi wa Umma na atafikishwa katika vyombo vya sheria badala ya kuendelea kuwakumbatia na kujenga Taifa la wezi, wasio na uwezo na mzigo Taifa.

Amewaasa wataalam hao kuacha kufundisha masomo kwa kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza kwani kwa kufanya hivyo kunapunguza umahiri wa lugha kwa watoto na walimu wenyewe.

Kuhusu suala la utoro amewataka watendaji hao kuchukua hatua kwani suala la utoro linakuwa sugu siku hadi siku na kwa hivi sasa kwa mujibu wa taasisi moja ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utoro wa walimu wa aina tofauti mashuleni umefikia asilimia 56 jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa taaluma nchini.

Bwana Salum Mohammed ni Mkuu wa shule ya Gungu sekondari amesema kikao hicho kilikuwa na tija na kwamba maagizo yote ya Serikali watayazingatia na kuyatekeleza mara moja, lakini ametoa ombi kwa Serikali kukumbuka kuwapandisha madaraja ili kuwamotisha walimu waweze kufanya kazi zao vizuri na kuleta matokeo chanya kwani ni muda mrefu madaraja hayo yalisimamishwa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda, amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma na kurejea Jijini Dodoma kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.

Baadhi ya Maafisa Elimu Wilaya Msingi na Sekondari, Maafisa Elimu Taaluma Msingi na Sekondari, Maafisa Vielelezo na Takwimu Msingi na Sekondari, Waratibu Elimu Kata, Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari, baadhi ya walimu wa msingi na sekondari na Wathibiti Ubora wa Elimu wakifuatilia hotuba ya mgeni Rasmi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *