Habari Kitaifa

Nimeridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa vituo vya afya nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakikata kwenye uzinduzi wa Kituo cha afya Mbonde kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, Mkoani Mtwara.

Na. Angela Msimbira MTWARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Joseph Pombe Magufuli ameipongeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa usimamizi  wenye weledi  katika ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za Afya Nchini.

Ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mbonde katika Halmashauri Mji wa Masasi, Mkoani Mtwara kwa niaba ya vituo 352 vya kutolea huduma nchini ambavyo vimejengwa katika Halmashauri zote nchini.

Mhe. Magufuli amesema kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma lakini Wizara hizo mbili zimeweza kusimamia kwa weledi utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo.

“Kutengwa kwa fedha ni sula la msingi lakini usimamizi wa fedha ni suala muhimu sana hivyo  nimeridhishwa na usimamizi uliofanywa na Wizara hizi mbili  ambapo ujenzi umefanyika kwa kiwango kikubwa na  usimamizi huo unaacha alama kwa nchi na kupunguza kero za miundominu ya afya nchini” Amesema Mhe. Magufuli

Mhe. Magufuli amewapongeza watumishi wa  OR-TAMISEMI  na Wizara ya Afya kwa kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia na kuhakikisha vituo vya afya vinakamilika kwa wakati na viwango vya juu na kuanza kutoa huduma kwa jamii ili kuwahudumia wananchi maskini nchini.

 “Panapostahili kupongezwa napongeza hadharani bila kificho na sitasubiri mpaka mtu afe, kwa kweli Wizara hizi mbili wamesimamia kazi ya ujenzi wa vituo vya afya kwa umakini mkubwa na wamefanyakazi nzuri” Amesisitiza Mhe. Magufuli

Amesema kuwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 wameweza kujenga Wodi ya Wazazi, Jengo la Maabara, Chumba cha kuifadhia maiti,  chumba cha Mionzi na Jengo la upasuaji hivyo nimeridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo katika Sekta ya afya

Mhe. Magufuli amewapongeza Wataalam wa afya nchini  kwa kufanyakazi kwa weledi na moyo wa kujitolea na kuwataka  kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii maskini ambao ndio wenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya nchini.

Aidha Mhe. Magufuli amefafanua kuwa gharama zilizotumika katika ujenzi wa vituo 352 ni shilingi bilioni 184 hivyo amewashukuru wananchi, wadau wa maendeleo kwa kujitoa kwa moyo  kuleta maendeleo katika Sekta ya afya nchini.

Wakati Huohuo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa sekta ya afya ni eneo linalogusa wananchi wa hali ya nchini hivyo serikali iliamua kuwekeza katika sekta ya afya ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Amesema tangu uhuru kulikuwa na Hospitali za Serikali 77 katika Halmashauri 185,  vituo vya afya 535 ambapo viliyokuwa na uwezo wa kufanya upasuaji ni  vituo vya afya 118  hali hii ilikuwa ikisababisha vifo vya mama na mtoto pale anapohitaji kujifungua kwa njia ya upasiaji kwa kuwa walikuwa wakitembea muda mrefu kufuata huduma hizo katika Hospitali za Rufaa.

Aidha amesema katika miezi 18 ya ujenzi wa vituo vya afya nchini Serikali imeweza kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya ambapo mpaka sasa vituo 352 vimeweza kujengwa na vinaweza kufanya huduma ya upasuaji.

Baadhi ya Watumishi wa Sekta ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo mara baada ya uzinduzi wa Kituo cha afya cha Mbonde kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi Mkoani Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa Kituo cha afya cha Mbonde kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Mbonde Mkoani Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha afya Mbonde kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, Mkoani Mtwara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *