Habari za Wizara

NMB Yaikabidhi Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Milioni 100

Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), pamoja na wawakilishi kutoka benki ya NMB kanda ya kati, wakiwa katika kikao cha makabidhiano ya fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kilichofanyika leo katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Jijini Dodoma kwa ajili ya kuwezesha Mkutano Mkuu wa jumuiya hiyo utakaofanyika wiki ijayo Jijini Dodoma.

Benki ya NMB imeikabidhi Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuufadhili Mkutano Mkuu wa 34 wa  jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo Jijini Dodoma.

Akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni mia moja kutoka benki ya NMB, mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gullamhafeez Mukadam ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo na kusema kuwa ALAT ni wabia wa benki hiyo hivyo wataendelea kudumisha mashirikiano yaliyopo.

Msaada huo unatokana na wito uliotolewa na ALAT mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu kupitia vyombo vya habari wa kuwakaribisha wadhamini mbalimbali watakaopenda kushiriki kwa lengo la kutangaza bidhaa na huduma walizonazo.

Mhe. Mukadam amesema masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa kawaida wa mwaka ni kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mikutano mikuu (yatokanayo), pamoja na kujadili taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli za Jumuiya.

Amesema agenda nyingine zitakazojadiliwa ni “Kupokea na kujadili taarifa ya fedha za Jumuiya ikiwa ni pamoja na kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Jumuiya kwa mwaka 2018/2019” Alisema MheMukadam.

Kwa upande wake Meneja wa NMB kanda ya Kati Nsolo Mlozi amesema msaada huo unatokana na umuhimu wa ALAT kwenye jamii na kwamba wataendelea kuboresha huduma zao ili kuendana na mahitaji ya watanzania hususani Serikali za Mitaa.

Amesema NMB inaendelea kushirikiana na ALAT kupitia halmashauri zaidi ya 160 ambazo tayari zimeshaingia kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia za kielektroniki, ambao umesaidia kuongeza mapato kupitia matawi 228, mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 800, na zaidi ya mawakala 6000 nchi nzima.

“Benki hii inaendelea kushirikiana na jamii, mfano kwa mwaka huu 2018, tulipanga kutoa misaada kwa jamii kupitia afya na elimu wenye zaidi ya shilingi bilioni moja, wafaidika wa moja kwa moja wa mchango huu ni halmashauri zetu, kwani madawati na vifaa tiba vinaenda kwa halmashauri” Amesema Mlozi.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 100 kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Gullamhafeez Mukadam, kwa ajili ya kuwezesha mkutano mkuu wa jumuiya hiyo utakaofanyika Tarehe 24 hadi 28 mwezi Septemba mwaka huu Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Gullamhafeez Mukadam akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha makabidhiano ya mfano wa hundi ya fedha yenye thamani ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na benki ya NMB kwa ajili ya kuwezesha Mkutano Mkuu wa jumuiya hiyo utakaofanyika wiki ijayo Jijini Dodoma.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *