Elimu

Nzunda Aagiza Kuacha Vitendo vya Udanganyifu Mitihani Kidato cha Nne

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI akikagua baadhi ya madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Kibondo wilayani Kibondo mkoani Kigoma. Kushoto kwake ni Mkuu wa shule hiyo Bi. Ruth Msweth

Na. Fred Kibano

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Elimu na Mamlaka za Elimu nchini kusimamia taaluma ili kumaliza tatizo la madawati na kudhibiti vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani.

Nzunda ametoa kauli hiyo alipotembelea shule ya sekondari ya wasichana Kibondo iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma ambapo amesema hivi karibuni kumekuwepo na vitendo vya udanganyifu katika mitihani kuanzia shule za msingi na sekondari jambo ambalo halitavumilika.

Nzunda amesema kuwa hatavumiliwa mtumishi yeyote yule atakayebainika kupokea rushwa na kufanya udanganyifu kwenye mitihani ikiwa ni pamoja na mitihani ya kidato cha nne inayoendelea hivi sasa nchini kote kwani kwa kufanya hivyo tunajenga Taifa la watu wasio na ushindani na wasio na maadili na wezi.

“katika mitihani ya kitaifa sitaki udanganyifu bali uadilifu, mtumishi yeyote atakaye jihusisha na udanganyifu na kubainika, huyo tutamwondoa katika Utumishi wa Umma, msifanye udanganyifu bali simamieni maadili”

Nzunda amesema tayari Maafisa Elimu4, Maafisa Taaluma 4, Waratibu Kata 19 na baadhi ya Wakuu wa shule wamechukuliwa hatua kwa kupatikana na hujuma katika mitihani nchini

Pia amewataka Maaafisa Elimu na Wakurugenzi nchini kuacha kuzalisha madeni mapya ya watumishi katika Mamlaka zao kwani kwa kufanya hivyo wanaipa Serikali mzigo mkubwa wa madeni jambo ambalo halitavumilika.

Katika ziara hiyo pia amewaagiza Maafisa Elimu na Wakurugenzi katika mikoa yenye miradi ya Equip pamoja na shule shikizi kuwa inahakikisha inamalizia miradi yote yakiwemo madarasa na madawati kwa wakati mara ili ifikapo januari, 2019 ili wanafunzi wote watakaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanaanza masomo mara moja.

Mkuu wa shule hiyo Bi. Ruth Msweth ameishukuru Serikali kupitia mradi wake wa kukarabati shule kongwe nchini kuwa umeondoa changamoto lukuki zilizokuwa zinawakabili kama vile kuwepo kwa maji mpaka mabwenini, ujenzi wa madarasa na maabara mpya, ukarabatim wa miundo mbinu mingine na kuendelea kutenga bajeti ya elimu bila malipo kwani inasaidia kuendesha taaluma bila shida yoyote.

Naibu Katibu Mkuu Tixon Nzunda (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI yupo mkoani Kigoma katika ziara yake ya kikazi akijionea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na miradi ya elimu na miradi ya kuboresha mazingira ya biashara (Local Investment Climate).

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *