Elimu

“OPRAS Iwe nyenzo ya Mikataba ya Utendaji kazi”  Nzunda

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia elimu OR-TAMISEMI Ndugu Tixon Nzunda, akifungua mafunzo ya maafisa elimu kutoka Wilaya na Mkoa wa Singida juu ya mfumo wa upimaji utendaji kazi kwa njia ya wazi OPRAS jijini Dodoma katika ukumbi wa Land Mark (Picha na Atley Kuni- OR-TAMISEMI)

 

Na. Atley Kuni, OR-TAMISEMI.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Tixon Nzunda, amesema imefika wakati Mfumo wa upimaji utendaji kazi uliowazi (Open Performance Review Appraisal System-OPRAS) kutumika kama nyenzo muhimu ya upimaji kazi wenye matokeo chanya.

Nzunda amesema hayo hivi leo alipokuwa akifungua, mafunzo ya siku mbili kwa Maofisa Elimu pamoja na Makatibu wa Tume ya Watumishi wa Walimu TSD jijini Dodoma kutoka Halmashauri za Mkoa wa Singida.

“Mtumishi wa umma anatakiwa kupimwa kwa kuangalia mambo mahususi muhimu katika utendaji wake kama, umahiri wake, ubunifu wake na weledi wa kutumia taaluma yake katika utekelezaji wa majukumu yake.”

Naibu Katibu Mkuu Nzunda, alisema OPRAS isitumike kama fimbo ya kuwaadhibu watumishi bali kuwasaidia kutatua changamoto ambazo zitabainishwa kulingana na kada husika na mazingira ya utendaji kazi.

Ameongeza kuwa katika mfumo wa zamani ambao ulikuwa wa siri, ulimnyima mtumishi kujua kile kinacho jazwa na msimamizi wake wa kazi hali iliyochangia baadhi ya wasimamizi kuwaadhibu watumishi kwa hila na chuki binafsi.

“Katika mfumo wa sasa, Mwajiri/msimamizi wa kazi na mwajiriwa watakaa pamoja na kukubaliana kulingana na vigezo vilivyokubalika kupitia fomu ya OPRAS na endapo hawatakubaliana watakwenda kwa msuluhishi” alisema Nzunda na kuongeza, “inawezekana mtumishi ameshindwa kufikia malengo kwa sababu amekwamishwa na kutokuwepo kwa nyenzo lakini wewe msimamizi unataka kumuadhibu. hiyo sio sahihi”.

Naibu Katibu Mkuu, amewataka Maafisa Elimu hao kukubali kubadilika na kuachana na dhana za kizamani za kuishi katika mifumo ya kizamani na badala yake wapokee mawazo chanya yatakayo saidia katika utendaji kazi.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Nzunda ametumia fursa hiyo kuwaonya watumishi walimu walio wezi wa mitihani na wale watakao bainika kufanya hivyo hatakuwa na simile nao.

“Tunataka kujenga heshma ya nchi, tunapojenga heshima ya nchi lazima suala la elimu lipewe kipaumbele muhimu, hatuwezi kuwafundisha watoto wetu kuwa wezi kuanzia darasa la saba halafu tunataka waingie katika soko la ushindani kimataifa hatutaweza”, alisisitiza Nzunda.

Nzunda ameahidi kulisimamia suala la wizi wa mitihani kwa juhudi zake zote na katika kipindi chake chote katika nafasi yake hiyo hatakuwa tayari kuona kadhia hiyo inajitokeza nakusema yeyote atakaye thubutu hatavumiliwa, sheria za kazi zitachukuliwa ikiwepo kufikishwa mahakamani.

“Wizi wa mitihani ni kosa la kimaadili, tukikukamata, mbali ya kukupeleka tume ya walimu kwa shauri la kiusuluhishi, hatutaishia hapo, tutahakikisha mbali ya kufukuzwa kazi tutakupeleka mahakamani na hatimaye ufungwe jela” alisema Nzunda.

Awali akitoa maelezo na malengo ya mafunzo, Mwakilishi kutoka Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma PS3 anayeshughulikia Rasilimali watu Geoffrey Lufumbi, alisema katika utafiti uliofanyika kuhusu OPRAS Mwezi February 2017, ilibainika asilimia 80 ya watumishi waliohojiwa walionesha kutofahamu jinsi ya kuweka malengo sahihi ya utendaji kazi.

“Katika tafiti tendaji tuliofanya kwenye mikoa miwili ya Dodoma na Iringa na Wilaya nne tulibaini kuwa asilimia 40 walikuwa hawajazi kabisa OPRAS, asilimia 75 walisema hawaoni faida ya OPRAS, aidha asilimia 100 ya Wakurugenzi waliohojiwa walisema hawajazi fomu za upimaji kazi uliowazi za OPRAS”. Alisema Lufumbi.

Lufumbi alisema ili mafunzo hayo yawe na tija ameomba Ofisi ya Rais TAMISEMI kupeleka maelekezo maalum kwenye Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya kwamba  ifikapo tarehe 05 Jamuari, 2019 Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi wawe wamewezeshwa kuwaelekeza walimu namna ya kujaza OPRAS kwa kufuata mwongozo ulioboreshwa.

Serikali ilianzisha matumizi ya mfumo wa upimaji kazi uliowazi na tathmini ya utendaji kazi kupitia waraka namba 2 wa 2004 na kufuta mfumo wa zamani ambao ulikuwa wa siri na wa vificho usiompa fursa mwajiriwa kutathiminiwa kwa uwazi na ambao ulikuwa ukizorotesha uwajibikaji katika utumshi wa umma.

Mwakilishi kutoka Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma PS3 anayeshughulikia Rasilimali watu Geoffrey Lufumbi, akitoa maelezo ya utangulizi juu ya madhumini ya mafunzo hayo
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Nelesi Mulungu akishukuru mara baada ya hotuba ya Mgeni rasmi
Mmoja ya wawezeshaji wa mafunzo hayo ya OPRAS Bibi Anyangise Lupembe, akitoa mada wakati wa mafunzo hayo ya siku mbili jijini Dodoma.
Bibi Dorine Lutahanamala, akiuchangia mada kwakutaka ufafanuzi wa juu mfumo wa OPRAS katika mafunzo yalioanza leo jijini Dodoma.
Washiriki wa mafunzo wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wakati akifungua mafunzo hayo ambapo washiriki hao watalazimika kwenda kuwafundisha walio chini yao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *