Mafunzo

OPRAS Ni njia Muhimu ya Kuleta Ufanisi wa Watumishi

Mkurugenzi wa Rasilimali watu kutoka Tume wa Utumishi wa Walimu Ndg Moses Chitanda akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Elimu wa Mkoa wa Manyara kuhusu Mfumo wa OPRAS yanayofanyika mkoani Dodoma

Na. Atley Kuni- OR TAMISEMI

Imeelezwa kuwa moja ya njia itakayowezesha taifa liweze kupiga hatua katika nyanja mbali mbali za maendeleo ni kwa taifa hilo kujiwekea mazingira ya kupima utendaji wa kazi kwa njia iliyo wazi na inayotoa nafasi kwa mtumishi kujitathmini mwenyewe.

Kauli hiyo imetolewa na Ndg Moses Chitanda (kwa niaba ya Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Bibi Winfrida Rutaindurwa) kwenye mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Elimu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya mfumo wa (Open Performance Review Appraisal System-OPRAS) kwa Mkoa wa Manyara yanayofanyika jijini Dodoma.

Ndg Chitanda alisema mataifa mengi yaliyoendelea yaliwekeza katika rasilimali watu ikiwemo katika kupima na kufanya tathmini, na hii imewezesha mataifa hayo kupiga hatua za kimaendeleo.

Chitanda alisema, kujituma, nidhamu sambamba na kupokea maelekezo ndio njia pekee inayomwezesha mtumishi wa umma kupiga hatua katika utendaji wake wa kazi.

Mkurugenzi huyo wa rasilimali watu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu alifafanua, katika hali ya sasa nchi inahitaji watu wabunifu na wachapa kazi ambao watapatikana kwa rasilimali watu kutekeleza mfumo wa OPRAS.

“Mafunzo haya ya OPRAS yatasaidia kuibua ubunifu na utendaji uliotukuka hivyo tutegemee matokeo chanya kwa walimu”.

Chitanda alisema, shabaha kuu ya kuanza na kada ya walimu kwenye kuboresha ujazaji wa malengo ya OPRAS ni kutokana na kundi hilo kuwa na majukumu mengi yanayo fanana lakini pia weledi na wepesi wakusaidia kuisambaza elimu hiyo kwa makundi na kada zingine.

“Ili kuwa na utekelezaji wa uhakika wa utaratibu ulioboreshwa, wadau walikubaliana kuchagua kada moja katika utumishi wa umma ili liwe kundi la kuanzia, kwa kutumia vigezo mbalimbali, alisema Chitanda na kuongeza ilikubaliwa zoezi lianzie kwa walimu ambao kwa mujibu wa kazi zao ni lenye majukumu ya aina moja ambayo yanaweza kupangwa kwa kutumia maelezo ya kazi ya kada ya walimu”.  Lakini pia ni rahisi kueneza elimu hii mpya ya upangaji malengo ya mtumishi”.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma, PS3 Geoffrey Lufumbi, alisema mafunzo hayo ni mwanzo wa mafunzo yanayotolewa nchi nzima kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kufuatiwa na walimu wote nchini.

Ndg Lufumbi alibainisha kuwa zoezi hili limefanikiwa kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu na PS3 kama sehemu mojawapo ya uimarishaji wa mifumo ya Rasilimali Watu kupitia Mradi wa PS3.  

“Maamuzi yote ya taasisi ikiwepo upangaji wa kazi na watumishi yatafanikiwa tu endapo OPRAS zitajazwa kwa ufasaha na itasaidia kutambua malengo kama yamefikiwa ama la”.

“Kama PS3 tunafanya kazi katika vipengele mbalimbali ikiwepo Utawala Bora, Mifumo ya TEHAMA, Mifumo ya Fedha, Tafiti tendaji pamoja na Rasiliamali Watu.

Akitoa mada katika kwenye mafunzo hayo ya siku mbili, mmoja ya wawezeshaji wa kitaifa wa OPRAS Ndg Samson Medda, alisema Mipango, malengo, dira na dhima ya taasisi vitafanikiwa kwa taasisi kuwa na OPRAS inayotekelezwa kwa umakini.

Katika Semina hiyo Ndugu Chitanda hakuacha kuwashukuru Watu wa marekani kupitia mradi wa uimarishaji wa mifumo ya sekta za umma PS3 kwa kazi kubwa wanayoifanya nchini yakuwezesha mifumo mbali mbali hususan ni imarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma.

Mpango wa watumishi kwa njia ya wazi umefafanuliwa kupitia,  Miongozo na Sheria mbali mbali za utumishi wa umma ikiwepo Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2007 kupitia Kifungu cha (3) cha marekebisho Namba 18 ya 2007 kinafafanua dhima ya Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Taasisi zinazojitegemea pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia fomu za OPRAS katika kupima utendaji wa watumishi waliopo chini yao.

Mshauri wa Rasilimali watu kutoka mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma PS3, Geoffrey Lufumbi, akitoa maelezo ya utangulizi kabla yakuanza kwa semina hiyo ya siku mbili jijini Dodoma
Mmoja ya Wawezeshaji wa Kitaifa kuhusu Mafunzo ya Mfumo wa OPRAS Nicodemas Tindwa akitoa mada katika Semina hiyo ya siku mbili jijini Dodoma.

 

Washiriki wa Mafunzo wakiwa katika picha ya Pamoja

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *