Habari za Wizara

OR TAMISEMI Yafunga Mwaka kwa Vituo 300 vya Afya kukarabatiwa

 

Jengo la wazazi katika kituo cha Afya Ikwiriri Moja ya Vitu vya Afya vilivyo karabatiwa kote nchini (Picha na Makta ya OR TAMISEMI)

Na. Atley Kuni- OR TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya OR TAMISEMI, Dkt. Zainab Chaula amewashukuru watumishi na wananchi kote nchini kutokana na ushirikiano wanao endelea kuutoa katika zoezi la ujenzi wa vituo vya afya ambapo hadi mwaka wa fedha unakamilika Juni 30, 2018 tayari wamesha karabati vituo 300.

“Asante kwa kutembea pamoja kwa matokeo chanya, tumefunga mwaka na ukarabati wa vituo 300, awamu ya kwanza ilikuwa Mwezi Oktoba, 2017 hadi Machi tulikarabati  vituo 44 kwa fedha za Mfuko wa afya (HBF)” alinukuliwa Naibu Katibu Mkuu

Dkt Chaula alisema katika awamu ya pili iliyoanza Januari hadi Mei, 2018 jumla ya vituo 139 kutoka fedha za Benki ya Dunia ziliwezesha ukarabati na vituo 100 vilikarabatiwa kupitia mfuko wa afya (Health Basket Fund-HBF),

Chaula alifafanua kuwa katika gawio la serikali kutoka benki ya  CRDB ni vituo 39 vimefanikiwa kukarabatiwa, huku taarifa hiyo ikitanabaisha zaidi kwamba, katika awamu ya tatu jumla ya vituo 27 vinaendelea kukarabatiwa, ukarabati ulio anza mwezi Mei na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2018.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa vituo 25 vimekarabatiwa kutoka fedha ya Mfuko wa Afya ilivyovuka mwaka 2016/17 na Vituo 2 vilitokana na fedha za DANIDA kwenye Mikoa 2 yenye Wakimbizi  ya Kigoma na Katavi.

Ameongeza kuwa katika awamu ya nne wamejipanga vilivyo kuhakikisha fedha iliyokwisha toka inafanyiwa kazi.

“Awamu ya Nne vituo vya Afya 89, Zahanati 10 , nyumba 10 za Watumishi sambamba na ukarabati wa Hospitali 5 za Wilaya, fedha yake imetoka mwishoni Mwa Mwezi wa Sita, 2018 na hizi ni fedha za LGDG”. Alisema Dkt Chaula.

Akihitimisha taarifa yake Dkt Chaula amemshukuru Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Selemani Said Jafo (Mb) kwa ufuatiliaji na maelekezo yenye tija ya karibu kutoka kwake yeye mwenyewe pamoja na  wasaidizi wake wote, na kusema kwamba, umoja na mshikamano ndio ulio wezesha kupata fedha hizo, huku akihimiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa kuendelea kutumia (Force Account). Lakini pia kuzingatia muda wa majuma 20 uliowekwa katika kukamilisha kazi kulingana na muongozo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *