Mafunzo

PS3 yaombwa iende mikoa yote Tanzania Bara

Afisa TEHAMA wa OR TAMISEMI Mfaume Mnokote akiwasilisha mada ya matumizi ya dawati la dharura kwa washiriki wa mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2 jijini Mwanza

Atley Kuni na Glady Mkuchu – Mwanza

Washiriki wa mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2 kutoka mikoa ambayo haitekelezi Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3), wameiomba Serikali ione namna itakavyoweza kukaa na wadau hao ili mradi uweze kuhudumia nchi nzima badala ya sasa ambapo upo katika Mikoa 13 na Halamshauri 93 pekee.

Ombi hilo limetolewa na waweka hazina pamoja wahasibu kutoka Halmashauri za mikoa ya Tabora na Geita ambao wamekuwepo katika mafunzo ya siku nne ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma (Epicor) Toleo 10.2, ambapo mara baada ya mafunzo hayo watendaji hao wataanza kuutumia mfumo huo ifikapo Julai mosi, 2018.

Mafunzo hayo ya Epicor 10.2 yameendeshwa na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), kwa kushirikiana na Mradi wa PS3 ambao unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).  Katika mafunzo hayo, Serikali imewagharamia washiriki kutoka mikoa ambayo haipo chini ya Mradi wa PS3.

Nicholaus John ni mweka hazina katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita; yeye anasema pamoja na uzuri wa mifumo lakini wanapendekeza kuwa mradi pia uweze kufikiria kufika katika mikoa mingine ili kuweza kuleta uwiano sawia katika utekelezaji wa mifumo ya umma.

Nicholaus anaongeza kuwa matunda ya ukusanyaji mzuri wa mapato katika Halmashauri zao umetokana na kuwa na mifumo imara ambayo inasimamiwa na TAMISEMI, lakini pia ufadhili kutoka kwa Serikali ya Marekani kupitia mradi wa PS3.

Akitoa maoni yake, Shani Mangesho ambaye ni Afisa Msimamizi wa Fedha katika mkoa wa Tabora anakiri kuwa PS3 imefanya kazi kubwa kwenye mifumo, lakini bado wanayo hamu ya kuona mradi huo unaongeza eneo la ufadhili.

“Shauku yetu ni kuona mradi huu unakwenda na kwenye maeneo mengine ya nchi, hasa kwenye mikoa ambayo haipo chini ya mradi, katika wakati wa sasa mnapokuwa na malengo yakusukuma ajenda ya mifumo katika sekta za umma, ili kuwa na uwiano wa utekelezaji wa ajenda sisi ambao tupo nje ya mradi vipo baadhi ya vitu tunadhani tunavikosa kama vile baadhi ya wekahazina wa mikoa iliyo nje ya mradi kutokuwa na uwezo ya kuingia na kutumia mfumo na kuumia” alisema Mangesho.

Mbali ya kuomba mradi huo uweze kwenda nchi nzima, waweka hazina hao na wahasibu hawakusita kuelezea furaha yao ya mabadiliko ya mara kwa mara yanayoendelea kufanywa na Serikali, hasa katika kuimarisha mifumo ya sekta ya umma.

Zablon Nashokigwa ambaye ni mweka hazina katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, anasema mafunzo ya Epicor 10.2 kwa wataalam wa kada za wahasibu yamekuja kwa wakati muafaka, kwakuwa mifumo mingi sasa itafungamanishwa na mfumo huo.

“Nawashukuru TAMISEMI na PS3 kwa kutujengea uwezo.  Hii kwetu itakuwa chachu ya uboreshaji wa shughuli zetu za kila siku, hasa katika eneo la upatikanaji wa taarifa kwa muda muafaka.  Kutokana na mfumo huu kuwa wa kimtandao (web-based), utamwezesha mtendaji kufanya kazi mahali popote ambapo yupo, tofauti na mfumo ambao tunakwenda kuachana nao ifikiapo Julai mosi,” amesema Nashokigwa.

Marietha Masanja kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita amesema: “Katika Epicor.10.2 hakutakuwa na hundi, isipokuwa malipo yote yatafanyika kwa mfumo wa (Tanzania Interbank Settlement System-TISS) ambayo imeunganishwa kwenye mfumo huu ulioboreshwa, hivyo itawaepusha wahasibu na jukumu la kubeba pesa taslimu,” amesema Marietha.

Mafunzo ya Epicor 10.2 yamefanyika kwa wahasibu, waweka hazina na maafisa ugavi kutoka Halmashauri zote nchini, pamoja na Wasimamizi wa Fedha kutoka Ofisi zote za Mikoa ya Tanzania Bara.

Mmoja ya washiriki wa Mafunzo ya Epicor 10.2 akitoa msaada wa kiufundi wakati wa mafunzo hayo
Bibi Shani Mangesho Ofisa Msimamizi wa fedha mwandamizi katika Mkoa wa Tabora akiwa katika mtihani wa kuwapima Wekahazina na Wahasibu wakati wa mafunzo ya Epicor 10.2 jijini Mwanza

 

Washiki wa Mafunzo, wakiwa wanamsikiliza kwa makini Mfaume Mnokote hayupo pichani wakati wa somo la Msaada wa dharura wakati wa mafunzo ya Epicor 10.2 mkoani Mwanza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *