Habari Kitaifa

Rorya Wamkosha Dkt. Gwajima, Mwenyewe awapa Tano

 

Na. Atley Kuni- OR-TAMISEMI, Mara

Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imefanya vizuri katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya unaondelea kujengwa hivi sasa, hali hiyo ilimlazimu Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, OR-TAMISEMI kutoa pongezi huku akiziagiza Halmashauri zingine kote nchini kuiga mfano wa Halmashauri hiyo ambapo siri kubwa ya mafanikio ya ujenzi uliofikia zaidi ya asilimia 80 yakiwa yametokana na umoja, mshikamano na maelewano baina ya viongozi wa Halmashauri na Wilaya.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu, alisema hatua kubwa iliyofikiwa haina budi kupongezwa na kila mpenda Maendeleo wa Nchi hii, kwani yapo maeneo mengi ya nchi ambayo yalipata fedha za awamu ya kwanza kama Rorya, bilioni 1.5, lakini mpaka hivi sasa wanabishana wapi Hospitali ijengwe huku wananchi wakiendelea kuteseka wapi wapate huduma.

“Nikiri waziwazi kwakweli nyie mmekuwa wa mfano sana na hali hii ndio kurejesha Fadhili kwa Rais wetu kipenzi cha watanzania Dkt. John Pombe Magufuli”, alisema Gwajima na kuongeza na “ninatamani wengine wakaijua siri hii ya mafanikio, kwakuwa kuna Halmashauri huko sehemu zingine tulizopita ni vituko vitupu, pesa wamepelekewa toka Januari lakini hadi leo wanashindana wapi ijengwe Hospitali,” alishangazwa Dkt. Gwajima.

Kwa upande wao viongozi na Wataalam wa Halmashauri hiyo, walisema siri kubwa ni mshikamano na maelewano baina yao wenyewe lakini pia mawazo kutoka kwa wataalam wastaafu.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya Simoni Chacha, alisema, kikubwa walichokifanya mara baada yakupokea fedha walikaa kwa pamoja na kuweka mikakati ya namna ya ujenzi utakavyo endeshwa na kwakiasi kikubwa waliwashirikisha baadhi ya wataalam wastaafu.

“Sisi Mhe. Naibu Katibu Mkuu, hatukutaka kujifungia ndani wenyewe tuliwahusisha wataalam wastaafu, lakini sisi Kamati ya Ulinzi na Usalama katika maeneo yote tulikubaliana lazima tuwasikilize wataalam kwa ushauri wao na sisi kama wasimamizi hatukupuuza ushauri wao” alisema Chacha.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya hiyo Charles Chacha, alisema mara kadhaa Mhandisi na Mganga Mkuu wa Wilaya na wataalam wenzao walipokutana na jambo likawatatiza, basi waliwaomba ushauri na walijadili kwa pamoja namna yakutatua tatizo.

“Mhe. Naibu Katibu Mkuu, kwakuwa hapakuwepo na muongozo wakuteua kamati baada ya mvutano niliamua kufanya maamuzi magumu ikiwapo hili lakuwashirikisha wataalam wastaafu akiwapo Afisa Ugavi wetu ambaye kila siku jukumu alilonalo ni jinsi gani anapokea vifaa na kuvitoa kwenye vitabu vyetu kwa utaratibu na kwakweli amekuwa msaada sana,” alisema Mkurugenzi.

Nao wataalama Wahandisi wanao simamia shughuli za ujenzi walisema, kufikia asilimia zaidi ya 85 ya ujenzi haikuwa kazi ndogo kwani kila mara wamekuwa wakifanya vikao eneo la kazi na kupitia kila kinachofanyika na wakifika mahali wakashindwa kuelewana wanakwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na   kwa aajili yakupata ushauri alisema Mhandisi wa Halmashauri hiyo.

Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, umefikia  asilimia zaidi ya 80 kwa majengo yote yaliyo elekezwa na serikali kujengwa, Majengo hayo ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje asilimia 88, jengo la Maabara asilimia 87, jengo la Mionzi asilimia 87, na jengo la uzazi asilimia 86. Majengo mengine ni jengo la ufuaji 87 pamoja na jengo la Utawala asilimia 84, huku wakitazamia kukamilisha asilimia zilizobakia ndani ya miezi miwili ijayo ili huduma kwa wananchi zianze kutolewa.  

Naibu Katibu Mkuu, yupo kwenye ziara yakukagua shughuli za Miradi ya Maendeleo hususan sekta ya afya, ambapo katika siku ya kwanza ametembelea Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Rorya, Kituo cha Afya Otegi, Hospitali ya Mji wa Tarime , kituo cha Afya Magoma na Kituo cha Afya Nyamwaga ambacho   kilisajiliwa kama zahanati lakini kwa sasa kutokana uhitaji na ukarabati mkubwa unaoendelea, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ameomba kipewe hadhi ya Hospitali ya Wilaya.

Naibu Katibu Mkuu akiwasalimia Wagonjwa katika kituo cha Afya Otegi ambacho nacho alikitembelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *