Video

Sera mpya ya Ugatuaji wa Madaraka kuzipa nguvu ya kiuchumi Serikali za Mitaa

Na Mathew Kwembe

Serikali imesema kuwa sera mpya ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi imezingatia katika kuzipa uwezo zaidi wa kiuchumi Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.

Sera hiyo ya Ugatuaji wa Madaraka inatarajiwa kuibadili sera ya sasa ambayo iliandaliwa takribani miaka 20 iliyopita, ambayo kutokana na mazingira ya sasa serikali imeona ipo haja ya kuibadili ili iendane na matarajio ya nchi ya kufikia maendeleo ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Akifungua kikao cha kujadili mapitio ya andiko la awali la sera ya Ugatuaji wa Madaraka (D by D) na taarifa ya mapitio ya mgawanyo wa majukumu kati ya Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Tixon Nzunda amesema sera mpya ya ugatuaji madaraka itaziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na nguvu zaidi kiuchumi na hivyo zitaweza kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alisema kuwa ikiwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaweza kuandaa mazingira bora ya kibiashara na kusimamia viwanda katika maeneo yao ni wazi kuwa huduma kwa wananchi zitaboreshwa.

“Mamlaka za Serikali za Mitaa zikiwa na uwezo wa kiuchumi, zikawa na uwezo wa kuandaa mazingira bora ya biashara, zikawa na uwezo wa kuandaa viwanda katika ngazi ya maisha yao, vitakwenda kubadilisha mfumo wa kilimo chetu, zitakwenda kufanya mabadiliko ya mfumo wa utoaji huduma, lakini pia zitakwenda kuongeza uzalishaji katika Nyanja zote,” alisisitiza.

Naibu Katibu Mkuu aliongeza kuwa serikali inalenga katika kuongeza nguvu ya kiuchumi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuziwezesha Mamlaka hizo kukusanya mapato makubwa na hivyo kuzifanya kutokuwa tegemezi katika utoaji wa huduma muhimu kwa mfano huduma za elimu, utoaji wa huduma za afya na utoaji wa huduma za maji, makazi na huduma nyinginezo muhimu kwa jamii.

“Tunataka kuwa na Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye nguvu ya kiuchumi ya kujiendesha zenyewe kiuchumi, kutoa huduma bora, lakini bila kusahau suala zima la utawala bora tukianzia kwenye suala zima la ushirikishwaji wa wananchi, kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na sauti ya kuzisimamia serikali katika ngazi za vijiji, vitongoji lakini pia wananchi wanakuwa na uwezo wa kushiriki kupanga maendeleo yanayohusu maisha yao katika Nyanja zote za kiuchumi na kijamii,” alisema Naibu Katibu Mkuu.

Pia Bwana Nzunda aliongeza kuwa mapendekezo ya rasimu ya sera hiyo mpya imesisitiza kuwa katika utawala bora watumishi wanakuwa na weledi, waadilifu na wenye uwezo wa kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na serikali kutokana na utekelezaji wa sera hiyo.

Mapema kabla ya kumkaribisha Naibu katibu Mkuu ili kufungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Kisekta kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt Andrew Komba alisema kuwa kikao hicho kinalenga kujadili,na kuchakata mapitio ya rasimu ya sera mpya ya ugatuaji wa madaraka kwa umma.

Alisema kuwa mapitio ya sera mpya ya Ugatuaji wa Madaraka yanalenga kuboresha sera ya sasa ya Ugatuaji wa Madaraka ambayo ilitayarishwa mwaka 1998ili iweze kuendana na mazingira ya sasa ya utendaji kazi katika Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Dkt Komba aliongeza kuwa  Serikali inataka sera mpya ijikite katika kuwaandaa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi.

Alisema kuwa Serikali za Mitaa ndani ya sera hii zinatazamiwa zisimamie mabadiliko ya kiuchumi jambo ambalo halikuwa likisimamiwa katika sera iliyopita.

“Mapendekezo ya rasimu ya sera hii yamezingatia katika kuhakikisha kuwa Serikali za Mitaa zinasimamia vizuri kilimo, Sera ya nchi ya viwanda ili kuendana na malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na viwanda ili kukuza uchumi, lakini vile vile ofisi ya Rais TAMISEMI mwaka jana ilikuja na tamko la kuwa na viwanda 100 kila mkoa,” alisema Dkt Komba na kuongeza kuwa:

“Tunataka Sekretarieti za Mikoa na  Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kusimamia uratibu wa uanzishwaji wa uchumi wa viwanda kwa kushirikisha sekta binafsi lakini vile vile kushirisha wadau wengine wa maendeleo”.

Kwa upande wake mmoja wa walioandaa rasimu ya andiko la sera hiyo Dkt Richard Mushi kutoka shirika lisilo la kiserikali la REPOA alisema kuwa katika siku za hivi karibuni Ofisi ya Rais TAMISEMI imejikuta ikishughulikia majukumu makubwa mfano afya  na elimu ambayo kimsingi hayamo katika sera ya sasa ya ugatuaji wa Madaraka lakini imeyaweka katika sera mpya ya ugatuaji.

Naye Mtaalamu wa Sera kutoka Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF Dkt Pius Chaya alisema kuwa UNICEF kama Shirika la Umoja wa Mataifa iliamua kufadhili mradi huo baada ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuona umuhimu wa kuhuisha sera ya ugatuaji ambayo iliandaliwa miaka 20 iliyopita.

Aliongeza kuwa UNICEF kama wadau wa maendeleo wana mchango mkubwa katika ushirikishwaji wa wananchi hasa katika ngazi ya chini kupitia Mamlaka zao za Serikali za Mitaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *