Habari za Wizara

Serikali haitapandisha hadhi kituo cha afya cha Dongobeshi

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Senkamba Kandege akijibu Maswali leo Bungeni Jijini Dodoma.

Na. Angela Msimbira BUNGE-DODOMA

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Josephat Senkamba Kandege amesema Serikali haitakipandisha hadhi kituo cha afya cha Dongobeshi kwa kuwa tayari imeshaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya YA Mbulu  inayojengwa katika eneo hilo.

Akijibu swali leo Bungeni  amesema kwa kutambua umuhimu wa kituo hicho Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa lengo la kuboresha miundombinu ambapo machi , 2018 ilitoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa  majengo ya wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, nyumba ya mtumishi na jengo la kuhifadhia maiti.

Mhe. Kandege amesema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inayojengwa  katika Tarafa ya Dongobeshi ambapo ikikamilika itapunguza msongamano wa wagonjwa kwenye Hospitali  ya  rufaa ya  Hydom.

Amefafanua kuwa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Hydom  na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa jamii inayoizunguka eneo la Dongobesh na wakazi wa maeneo ya jirani wakiwemo wananchi wa Kata ya Gudhim, Yaeda na Ampatumat.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kuongeza watumishi katika Kituo cha afya cha Dongobesh ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 watumishi wapya 6 wameajiriwa na kufanya kituo kuwa na jumla ya watumishi 37 lengo likiwa ni kutoa huduma bora za afya kwa jamii.

Aidha Serikali imepeleka shilingi milioni 320 kwa ajili ya ununuzi   was dawa na vifaa tiba ambapo hadi sasa vifaa vya shilingi milioni 73 vimepokelewa katika  kituo hicho cha afya  ili kuboresha huduma za afya nchini.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *