Habari za Wizara

Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwenye Halmashauri

 

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Waitara (Mb) akijibu maswali leo Bungeni Jijini Dodoma.

Na. Angela Msimbira BUNGE – DODOMA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Waitara (Mb) amesema Serikali iliweka kigezo cha upimaji wa Halmashauri ili kuziwezesha kupata ruzuku ya maendeleo isiyo na masharti “Capital Development Grant Assessment”.

Akijibu hoja Bungeni leo amesema  miongoni mwa  vigezo  vilivyozingatiwa katika utoaji wa ruzuku ya maendeleo ni uwazi  katika mapokezi  na matumizi ya fedha kwenye ngazi ya vijiji, Kata na Mitaa kwa kuhakikisha mapato na matumizi  yanabandikwa kwenye mbao za matangazo.

Mhe. Waitara amesema kuwa mradi huo ulitekelezwa kupitia  fedha za wafadhili  kwa kushirikiana na Serikali  na ulifika kikomo  mwaka 2013 na Serikali  iliendelea kutekeleza miradi hiyo kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2017/2018.

Mhe. Waitara amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziwezesha  kutekeleza miradi ya maendeleo katika Sekta mbalimbali  zikiwemo za afya na elimu na wananchi wanachangia  nguvu kazi  na vifaa mbalimbali  kwa ajili ya ukamilishaji  wa miradi hiyo.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Leah Jeremeah Komanya  Mbunge viti maalum aliyetaka kujua Serikali imejipanga vipi  katika kuwachukulia hatua wakurugenzi wa Halmashauri wanaoshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato Mhe Waitara amesema kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha wanasiamamia na kufuatilia miradi ya mendeleo  inayotekelezwa katika Halmashauri  na kuwachukulia hatua Wakurugenzi wote wanaoshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zao.

“ Serikali imejiwekea utaratibu wa kutoa tathmini ya hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zote nchini na kuzipanga kulingana na ukusanyaji wa mapato lengo ni kuhakikisha kila Halmashauri inafika malengo yaliyopangwa ” Amesisitiza Mhe. Waitara

Aidha Serikali inakubaliana na suala la kuzipima Halmashauri  katika matumizi  ya ruzuku zinazotolewa na Serikali  na mjadala  unaendelea  ili kuona namna bora  ya kulitekeleza katika kuhakikisha  kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwenye Halmashauri  hadi ngazi  za vijiji

.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *