Elimu

Serikali kuajiri walimu 6000 mwaka huu

Na Mathew Kwembe, Chemba

Serikali imesema kuwa mwaka huu inatarajia kuajiri walimu wapya 6000 wa masomo ya Sayansi na Hesabu ambapo tayari kibali cha kuwaajiri walimu hao kimekwishatolewa.

Aidha Serikali inakusudia kuwapeleka walimu 11,000 wa masomo ya sanaa ambao ni wa ziada waliokuwa wakifundisha shule za sekondari kufundisha shule za msingi ili kukabiliana na upungufu wa walimu unaozikabili shule za msingi nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Mwita Waitara ameyasema hayo jana katika Wilaya Chemba, mkoani Dodoma wakati akizungumza na watumishi kutoka Idara za Elimu ya Msingi na Sekondari kutoka Halmashauri hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Mwita Waitara

Kauli hiyo ya Serikali inafuatia taarifa ya Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Chemba bwana Josephat Ambilikile kumweleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri ya Chemba ina upungufu wa walimu 808 kati ya walimu 1628 wanaotakiwa kufundisha katika shule za msingi 103 zilizopo katika wilaya hiyo.

Mhe.Waitara alisisitiza kuwa Serikali kuanzia mwaka huu itakuwa ikiajiri walimu kila mwaka ili kufidia walimu wanaostaafu na pia kukabiliana na upungufu unaotokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi kutokana na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto wao shule kufuatia uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kutoa elimu ya bila malipo.

“Tayari Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amekubali walimu waajiriwe na kibali kimekwishatolewa hivyo walimu 6000 wa masomo ya sayansi na hesabu na pia walimu 11,000 ambao ni walimu wa ziada waliokuwa wakifundisha masomo ya sanaa katika shule za sekondari watapelekwa kufundisha shule za msingi,” alisema Mhe.Waitara.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe.Mwita Waitara alipo tembea Halmashauri ya Chemba hivi karibuni

Pamoja na kueleza juhudi hizo za serikali za kuongeza idadi ya walimu, Naibu Waziri aliwataka walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na hesabu kutowakatisha tamaa wanafunzi wanapowafundisha wanafunzi masomo hayo badala yake watumie mbinu rahisi ili wanafunzi waelewe kwa urahisi masomo hayo.

“Tunatarajia Walimu wanapaswa kutumia mbinu rahisi wanapofundisha hesabu ili wanafunzi wapende somo hilo,” alisema na kuongeza:

“Hata utunzi wa vitabu vya kufundishia masomo hayo inabidi uangaliwe upya kwani watoto wanakimbia kusoma masomo ya sayansi na hesabu kwani kutokana na namna vitabu hivyo vinavyotungwa vinasababisha watoto wachukie masomo ya sayansi na hesabu,” alisema Waitara.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mwita Waitara anayeshughulikia, Elimu akizungumza na wananfunzi katika moja ya shule kwenye Halmashauri ya Chemba wakati wa ziara yake yakujionea maendeleo ya elimu wilani humo

Jambo lingine alilolizungumzia Naibu Waziri ni kiwango duni cha ufaulu kilichoonyeshwa na Mkoa wa Dodoma hasa wilaya ya Chemba katika matokeo ya kitaifa ya darasa la saba na kidato cha nne ambapo aliwataka watendaji wa elimu katika halmashauri hiyo kuja na mikakati itakayoboresha elimu wilayani humo.

“Ukitaja wilaya 10 zilizofanya vibaya kwa ufaulu Chemba ni ya 10 kwa matokeo ya darasa la saba, mkae chini mje na mkakati wa kuboresha matokeo ya wilaya yenu, cha muhimu mikakati hiyo ishirikishe ngazi zote kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, tarafa hadi kata,” alisema.

Baadhi ya Wanafunzi walipokuwa wakimlaki Naibu Waziri Mwita Waitara, alipofanya ziara katika Shule hiyo iliyopo Halmashauri ya Chema kujionea maendeo ya elimu

Pia Naibu Waziri alikemea tabia iliyojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya watendaji wa elimu kushiriki katika kuiba mitihani ambapo aliagiza kuwa kama kuna mwalimu ameshiriki katika wizi wa mitihani halmashauri isisite kumchukulia hatua kwani kitendo hicho kinarudisha nyuma maendeleo ya elimu ya nchi.

Sambamba na hilo Mhe.Waitara alionya tabia ya baadhi ya watendaji wasio waaminifu katika halmashauri kutumia kinyume na maelekezo ya serikali fedha za miradi kwa ajili ya kusaidia miundombinu ya shule.

“Fedha kama ni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ipokee na iende ikajenge hosteli, kadhalika kama fedha ni kwa ajili ya kununulia samani za shule ipokee na iende ikanunue samani za shule, ukigusa fedha ya elimu kinyume na maelekezo ya serikali tutashughulika na wewe,” alionya Waitara.;

Mapema Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea shule ya sekondari na shule ya msingi ya Chemba na kushuhudia ujenzi unaoendelea wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya sekondari chemba, ujenzi ambao umetokana na michango ya wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mheshimiwa Simon Odunga alimweleza Naibu Waziri kuwa  wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa walimu na kukosekana kwa utayari kwa jamii kuchangia masuala ya elimu kwa dhana kuwa kila kitu kinatolewa bure na serikali.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *