Afya

Serikali Kubuni Mbinu Mpya za Kudhibiti Malaria nchini

Na Fred Kibano

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe amewataka Wadau wa afya kuhakikisha mipango ya kupingana na malaria nchini inafanikiwa kwa kutumia mbinu stahiki na kwa wakati badala ya kutumia mbinu za siku zote zisizo leta matokeo chanya.  

Mhandisi Iyombe ameyasema hayo Jijini Dodoma leo wakati akifungua mkutano wa pamoja wa Watendaji wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Viongozi wa Mradi wa Vector Works unahusiana na ugonjwa wa malaria wenye lengo la kujadili utekelezaji wa mradi huo kulingana na vipaumbele vya Serikali.

Iyombe amesema tusiwekeze fedha nyingi katika kugawa vyandarua badala ya kununua viatilifu (dawa za kuua mazalia yote ya mbu) vitakavyotumika kuua mbu kwenye maskani yao lakini pia amewataka wajumbe kufanya tafiti na vikao vyenye kuleta matokeo na kufanya makubaliano ambayo yatawasaidia wananchi ambao ndio lengo kubwa.

“Kumekuwepo na tafiti nyingi za malaria na baadhi zinasema kuwa malaria inapungua kitu ambacho kiuhalisia sio kweli kwani malaria ipo na inaendelea kuwaua watanzania, kama tunataka kumaliza tatizo la malaria basi hao mbu tuwafuate kule kule wanapozaliana, tuwaangamize kulekule wanapozaliana”

Iyombe amewataka wajumbe hao wabadilike na kuelekeza hali halisi iliyopo katika Halmashauri na Mikoa na pia kuelekeza vitu ambavyo vitaleta matokeo chanya kwa haraka.

Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Dkt. Zainab Chaula amesema lengo la wizara ni kuondoa kabisa malaria na ili tuwe timu moja lazima tuwe  na mkakati wa pamoja kwa maana ya wadau na Serikali kushikana mkono na kutembea pamoja kwani Sera ya malaria inayoandaliwa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria ndiyo inayotumika katika nchi nzima

Amesema Usimamizi na Utekelezaji wa Sera hiyo upo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na ndio maana Wadau wote lazima wapitie wizarani ili kujua wanachoenda kufanya kwa wananchi kama mkakati wa pamoja na sio kila mmoja anajiamulia jambo lake.

Naye Mratibu wa Taifa wa malaria Dkt. Ally Mohammed amesema tayari wameweka mikakati kwa ajili ya kudhibiti malaria nchini kwani Halmashauri kwa sasa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya malaria katika mwaka huu wa fedha nah ii ni moja ya mafanikio makubwa.

Dkt. Ally ametaka Wadau na Serikali kuendelea kushirikiana pamoja katika kuufanyia kazi mpango kazi wa malaria kwani malaria bado ipo na hivi sasa hali ya malaria nchini ni asilimia 10 kwa tathmini ya mikoa yote lakini lengo la mpango wa Taifa ilikuwa kufikia asilimia 5 mwaka 2017 lakini kwa sasa ni asilimia 7.3 ijapokuwa kwa kiasi kikubwa malaria imepungua na nchi imepiga hatua.

Kwa upande wake Mratibu wa Malaria Taifa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Stella Kajange amesema kwa kuwa wote tunajenga nyumba moja, kila mmoja atimize majukumu yake na pia ametoa wito kwa Watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wajue Zaidi matatizo yao ili katika hatua ya utekelezaji vipaumbele vyao vya malaria viweze kufanyiwa kazi badala ya kusubiri watafiti na wataalam ambao hawatoki maeneo yao.

Naomi Serbate Mtaalam Msimamizi wa Mradi wa Afya USAID Tanzania amesema Mradi wa malaria Tanzania unafadhiliwa na Chuo Kikuu cha John Hopkins na wanaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kufanya tafiti, kuboresha Sera na kuamua kwa pamoja ni namna gani tufanye ili tusonge mbele.

Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Dkt. Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Viongozi wa Mradi wa Vector Works unahusiana na ugonjwa wa malaria katika Ofisi za OR TAMISEMI Jijini Dodoma leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *