Elimu

Serikali Kuendelea kukarabati shule Kongwe

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Joseph Kakunda akiongea na wanafuzi (hawapo pichani) wa shule ya sekondari Kilosa ambapo aliwataka wasome kwa bidii na kuahidi kukarabati majengo na kujenga majengo mapya ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia

Na. Fred Kibano

Serikali imesema itaendelea kukarabati shule kongwe nchini ili kuendelea kutoa mchango wake katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Joseph Kakunda ameyasema hayo jana alipotembelea shule ya sekondari Kilosa, na kuahidi kuendelea kuboresha shule hiyo na kwamba katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 230 ili kuongeza miundombinu.

“shule hii inahitaji ukarabati mkubwa, tutahakikisha shule hii inafanyiwa ukarabati mkubwa, hapa shuleni Kilosa tumepanga kuleta shilingi milioni 230 ili zisaidie kujenga madarasa 4 na mabweni 2 ili mazingira yawe bora, hayo ndiyo tunayoyashughulikia,”  alisistiza Kakunda.

Amesema Serikali kupitia mkakati wake wa kuboresha shule za sekondari nchini, tayari jumla ya shule za sekondazri 3,159 zimekwisha karabatiwa kwa kuboresha madarasa, mabwalo, majiko, stoo, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine.

Amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa kutumia mbinu zao na mbinu wanazopewa na walimu wao lakini pia amewataka kuboresha upendo kwa wanafunzi wenzao wenye ulemavu ambao wanasoma shuleni hapo kama familia moja.

Katika kuelekea Tanzania ya viwanda, ameutaka uongozi wa shule kuandika andiko litakaloonyesha kulima mazao ya alizeti na kuanzisha kiwanda kidogo cha kukamua alizeti ili wanafunzi hao waweze kujifunza na kupata ujuzi.

 Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Kilosa, Mbaraka Kupela, amesema shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi kidato cha sita, inakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya bweni 1, madarasa 10, matundu ya vyoo 4, maabara 2, nyumba za walimu 19, maktaba 1, bwalo 1, mabweni 2 na maabara ya kompyuta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *