Elimu

Serikali Kuwachukulia Hatua Wanaochepusha Fedha za Miradi ya Equip T

Baadhi ya washiriki waliohudhuria kikao kazi cha Wadau, Wataalam na watendaji cha Equip T Jijini Dodoma leo.

Na. Fred Kibano

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – ELIMU (OR – TAMISEMI) Tickson Nzunda amewaonya Watumishi wa Serikali watakaobadilisha matumizi ya fedha za miradi kwa kuzipeleka katika matumizi mengine watashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria.

Akitoa hotuba yake wakati wa kufungua mkutano wa siku mbili wa Wadau wa Elimu Tanzania wanaotekeleza mradi wa Equip T Jijini Dodoma, Nzunda amesema Serikali haitawaacha watumishi waliopewa jukumu la kusimamia fedha za miradi lakini wao wanafanya matumizi mengine yasiyohusiana na mradi.

“Kwa wale watakaotumia vibaya au kubadilisha matumizi fedha za miradi mbalimbali zilizotolewa, hatua kali za kinidhamu na sheria zitachuliwa kwa wahusika bila kumwonea aibu”alisema Nzunda.

Aidha, amesema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuwa ikisisitiza kuwa kila rasilimali fedha inayotolewa inaenda kuimarisha eneo husika hivyo fedha zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alifafanua kauli hiyo kwa kutoa mfano wa watumishi wawili kutoka Wilaya ya Butiama Mkoani Mara na mwingine kutoka Mkoa wa Iringa walihamisha matumizi ya fedha na Serikali imechukua hatua ya kuwasimamisha kazi mpaka wahakikishe wanazirudisha fedha hizo kabla ya Machi 30 mwaka huu.

 Akitaja mafanikio ya Mradi wa Equip T, Nzunda amesema mradi umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi  nchini, umeweza kumalizia ujenzi wa vyumba vya  madarasa 251 yanayotokana na nguvu za wananchi  katika mikoa tisa ya Equip T, umewezesha mafunzo kwa Waalimu 61,000 kwa kufundisha njia bora za ufundishaji katika madarasa yenye idadi kubwa ya wanafunzi, pia uimarisha mahudhurio ya wanafunzi na kupenda shule mradi huo umetoa hamasa kwa watoto yatima  na wanaoishi kwenye mazingira magumu kuandikishwa shule, umewezesha kuanda takwimu na kuweka mfumo wa ufuatiliaji kwa mikoa 13 kuanzia ngazi ya Kata hadi kufikia Mkoa .

Naye Mkuu wa kitengo cha huduma za  Jamii  shirika la Uingereza linalofadhili mradi huo (DFID) Getrude Mapunda alisema shirika hilo lilitoa shilingi bilioni 180 kwa ajili ya kufadhili mradi kwa miaka sita nchini.

Mapunda alisema mradi wenye lengo la kusaidia kuinua elimu Nchini ulianza mwaka 2016 na unatarajiwa kufikia ukomo mapema mwaka 2020.

Alisema lengo la kukutana na watekelezaji wa mradi wa Equip T ni pamoja na wafadhili kujadili mafanikio na changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi huo.

Hata hivyo alisema wafadhili wamefurahishwa kutokana na Serikali kuwawajibisha watumishi waliohamisha fedha za mradi kwa matumizi mengine.

“Sio kwamba fedha zimeibiwa, hapana, ila isipokuwa zilihamishwa na kutumika kwa shughuli zingine nje ya malengo ya mradi wa Equip Tanzania” alisema Bi. Mapunda.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge amesema mradi wa Equip T umesaidia wanafunzi wa shule za msingi na wao kama Serikali mkoani Lindi wameweza kuchukua hatua za utekelezaji wake kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuanzisha kampeni maalum, “msaidie asome, mimba baadae”, ambayo inalenga mtoto wa kike kusoma na kumaliza masomo yake kwani kundi kubwa la watoto linaishia njiani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *