Habari za Wizara

Serikali, PS.3 Wapongezwa Misungwi

Selemani Mtinangi Afisa Takwimu kutoka OR-TAMISEMI, akitoa tathmini ya jumla mara baada yakukamilisha shughuli ya iMES na kwenda uwandani mkoani Mwanza

Na. Atley Kuni- TAMISEMI

Watendaji katika Halmashauri ya Misungwi mkoani Mwanza wamepongeza juhudi zilizochukuliwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI pamoja na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma nchini PS.3, kufuatia kukamilisha uundwaji wa mfumo jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathimini (integrated Monitoring and Evaluation System- iMES) ambao utawezesha kupata taarifa na takwimu katoka jukwaa moja.

Pongezi hizo zimekuja wakati huu ambao Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwakushirikiana na Wizara za kiseta pamoja na Wadau wa Maendeleo nchini USAID, kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma nchini kukamilisha utengenezaji wa mfumo wa iMES ambao unalengo lakutatua tatizo la upatikanaji wa taarifa na takwimu kwaajili yakufanya maamuzi kwenye mipango ya maendeleo.

Akiongea wakati wa Majaribio ya Mfumo huo, Mwalimu Meshack Chaula, ambaye amekuwa kwenye dawati la takwimu katika Halmashauri ya Misungwi kwa kipindi cha Mwaka mmoja, amesema hapo awali walikuwa na kasoro ndogo ndogo za kimfumo hasa kutokana na kutokuwepo kwa jukwaa moja ambalo lingekuwezesha kuona takwimu zakutoka sekta nyingine lakini sasa iMES imekuja kutoa suluhu.

“Lazima tukiri kuwa, Serikali inafanya kazi nzuri na katika hili tunajionea kazi kubwa katika mifumo mbalimbali, sote tunajua tatizo la taarifa na takwimu katika nchi yetu,   mfano mdogo ni hapa katika Halmashauri yetu tuliletewa fedha za kukamilisha maboma ya vyumba vya madarasa mawili  kwa kila shule, lakini katika ile orodha iliyokwenda ngazi za juu zilikuwepo shule mbili hazikuwa na sifa za vyumba viwili, suala hili lilitokana na kutokuwa na dashboard moja ya taarifa, alisema Chaula.

Mbali na kupongeza, wataalam hao wanaiona iMES kuwa Mfumo utakao mrahisishia mtumaji wa taarifa pindi zinapo hitajika muda wowote, kutokana na kwamba ni   web Based system.

“Kwa iMES, unaweza kutuma taarifa hata ukiwa njiani ili mradi uwe na kifurushi cha mtandao kwenye kishkwambi au simu janja yako” anasema Chaula na kusisitiza kuwa, kuna wakati mtu anaombwa taarifa akiwa hajajiandaa, hivyo baadhi ya taarifa   zikawa zinatumwa bila usahihi kutokana kuwa na vyanzo tofauti tofauti lakini kwakuwa sasa taarifa zote zitapatikana kwenye jukwa moja ni imani yetu kukinzana kwa takwimu hakutakuwepo.

Kwa upande wake, Katibu wa Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi bibi Swaiba Ngulugulu pamoja na kupongeza, yeye ameelekeza maombi yake kwa watengenezaji juu ya taarifa za mfumo wa DHIS-2 na mifumo mingine kama FFARS na Epicor kuvutwa katika mfumo wa iMES ili kuondoa kujirudiarudia kwa ujazaji wa takwimu, alisema  Swaiba.

“Tutafarijika kuona takwimu za Mifumo mingine zinavutwa moja kwa moja kwakuwa mambo mengi tunayo yajaza ni yale yale tu, mfano taarifa za fedha, taarifa watumishi, kwakutaja kwa uchache.” alihitimisha Swaiba.   

Mkoa wa Mwanza na Halmashauri zake za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, zimekuwa Halmashari za mwanzo kabisa kuanza kuutumia mfumo ambapo jumla ya watumiaji 63 kutoka sekta tofauti tofauti wamewezeshwa kuanza kuutumia mfumo wa iMES.

 

  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *